NA MWANDISHI WETU,ARUSHA
NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis amekitaka kiwanda cha nguo cha A to Z kilichpo mkoani Arusha kikamilishe ujenzi wa mtambo wa kutibu majitaka ndani ya miezi miwili.
Khamis ametoa maelekezo hayo Septemba 20,2022 jijini Arusha wakati alipofanya ziara ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuhusu kuondoa changamoto ya harufu na majitaka yanayotirirka kupita mtaro unaopita kwenye makazi ya watu.
Hata hivyo Khamis ameelekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini, wataalamu wa mazingira kutoka Ofisi za Mkuu wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri ya Jiji la Arusha kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha maeleekzo hayo yanatekelezwa.
“Hamuwezi kujua hizi harufu mbaya za haya majitaka yanayotoka hapa na kutiririka kwenye makazi ya watu zina athari gani, sasa ninatoa miezi miwili mkamilishe mtambo wa huu,” amesema Khamis.
Aidha,Khamis amebainisha kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikilamikiwa na wanachi kwa muda mrefu kwa uchafuzi wa mazingira kwa kutiririsha majitaka katika makazi ya wananchi.
Amesema Serikali inawapenda wawekezaji lakini wakati huohuo inalinda afya za wananchi wake pamoja na hifadhi ya mazingira lakini kiwanda hicho kimekuwa kikilamikiwa na wananchi kuhusu kuchafua mazingira.
Awali Meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini Lewis Nzali amesema baraza hilo limekuwa likitoa maelekezo mbalimbali ikiwemo kukipiga kiwanda hicho faini kwa uharibifu wa mazingira.
Nzali amebainisha kuwa kutokana na hatua hizo kiwanda cha A to Z kimeweza kuanza kujenga mtambo wa kuchakata majitaka kabla ya kwenda kwenye mazingira.
Nzali ameongeza kuwa hatua hiyo imeleta mafanikio katika sekta ya uwekezaji nchini kwa kuweza kuzingatia Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.
Kwa upande wake Meneja wa Kiwanda cha A to Z Sylivester Kazi ameahidi kukamilika kwa ujenzi wa mtambo huo ili kulinda afya za wananchi wanaozunguka eneo hilo.
Mtambo huo umegharimu kiasi cha sh. Bilioni moja ambapo kukamilika kwake kutaondoa tatizo la majitaka kutiririka katika makazi ya wanachi na kusambaa kwa harufu mbaya.




Discussion about this post