NA MWANDISHI WETU ,ARUSHA
SERIKALI imesema takribani dola za kimarekani Bilioni 19.2 za kimarekani zitatumika katika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na mabadiliko tabianchi.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 3,2022 jijini Arusha na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt.Selemani Jafo amesema hayo leo katika kikao cha wadau wa Mazingira kujadili mikakati ya nchi kuongeza uwezo wa kupata fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema Serikali inachukua hatua kubwa kama vile kuandaa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi 2021, Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2023) na Miongozo na Kanuni za Biashara ya Kaboni, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Tanzania pia imetekeleza miradi mbalimbali ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kuta katika fukwe mkoani Mtwara na visiwani Zanzibar pamoja na miradi mingine katika Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Nishati, Misitu, Viwanda, TEHAMA pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi” amesema Dkt. Jafo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Omar Shajak amesema kwa upande wa Zanzibar kikao kazi hiki pia kitaweka mikakati ya kupata fedha zitakazotumika pande zote mbili za Muungano
Naye Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba amesema kwa muda wa siku nne Mashirika ya Kitaifa, Asasi za Kiraia na taasisi za kifedha pamoja na mambo mengine watapitia msimamo wa Tanzania kuelekea Mkutano wa 27 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika Novemba 6 hadi 18,2022 nchini Misri.




Discussion about this post