NA MIRIAM SARAKIKYA,ARUSHA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Sh.Bilioni mbili ili kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani Arusha katika Jiji la Arusha.
Hayo yameelezwa Oktoba 6,2022 jijini Arusha na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda wakati akizungumza na wakuu wa shule za sekondari za jiji hilo.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kiasi cha Sh.Bilioni mbili kwa wilaya hiyo ili kuongeza kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaofaulu wanapata nafasi ya kuendelea na masomo.
“Fedha hizi zitatumika kujenga vyumba vya madarasa ili ifikapo mwaka 2023 wanafunzi wote watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wawe wamejiunga,na shule 20 za wilaya hiyo zitanufaika na fedha hizo”amesema Mtanda
Hata hivyo Mtanda ametoa siku 75 kwa wakuu wa shule kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa na fedha hizo zifanye kazi kwa wakati na siku hizo zitakapoisha kila mkuu wa shule anatakiwa kukabidhi kwa Serikali .
Ameongeza kuwa hata wavumilia wale wote watakaokwamisha zoezi hilo la mradi kukamilika kwa wakati na ni muhimu kwa wakuu wa shule kuunda Kamati za Ujenzi wa Vyumba vya Madarasa ili kusimamia mradi huo .
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Agney Chitukuro amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia kiasi hicho cha fedha na kuwataka wakuu wa shule kusimamia fedha hizo ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Kiasi hicho cha Sh.Bilioni mbili zilizopokelewa katika halmashauri ya jiji hilo zitatumika kujenga vyumba vya madarasa 100 katika shule 20.




Discussion about this post