NA MWANDISHI WETU,ARUSHA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika (65th UNWTO-CAF Meeting) unaoanza leo Oktoba 5, 2022 jijini Arusha.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Arusha.
Amesema lengo la mkutano huo ni kujadili kuhusu mustakabali wa ustawi wa maendeleo ya sekta ya utalii barani Afrika hasa baada ya athari za mlipuko wa janga la ugonjwa wa UVIKO-19 uliokuwa umeathiri utalii wa kimataifa kwa wastani wa kati ya asilimia 50 hadi 85 katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Aidha, ameongeza kuwa mkutano huo ni muhimu kwa kuwa ni mojawapo ya jitihada za Serikali katika kuongeza idadi ya watalii na kutanua wigo wa mazao ya utalii nchini kupitia uendelezaji wa mazao ya utalii ya kimkakati hususani Utalii wa Mikutano na Matukio.
Balozi,Dkt.Chana amefafanuwa kuwa mkutano huo utawezesha kujengea uwezo wataalam na wadau wa utalii katika kutangaza utalii, kuendeleza na kufungamanisha mazao ya utalii katika kanda mbalimbali za utalii nchini kulingana na shabaha ya kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni tano na mapato ya Dola za Marekani Bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.
“Mkutano huo ni nyenzo mojawapo ya kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,katika kutangaza utalii ndani na nje ya nchi kupitia programu ya Tanzania – The Royal Tour”amesema Balozi Dkt. Chana.

Mkutano huo wenye Kauli Mbiu ya “Kuujenga Upya Utalii Stahimilivu wa Afrika kwa Maendeleo Jumuishi ya Kiuchumi na Kijamii”. utahudhuriwa na Katibu Mkuu wa Shirika hilo Zurab Pololikashvili na kukutanisha mawaziri wenye dhamana ya masuala ya utalii na maliasili kutoka nchi wanachama wa UNWTO wa Kanda ya Afrika zaidi ya 50.
Mbali na hao lakini pia wadau wengine wakiwemo wataalam wa utalii na ukarimu katika ngazi ya kimataifa na kikanda, watoa huduma mbalimbali katika mnyororo wa utalii, wawekezaji, pamoja na watu mashuhuri zaidi ya 150.




Discussion about this post