NA MWANDISHI WETU,DODOMA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku 15 kwa Kampuni ya Inter Country Contractors kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa miradi ya barabara katika Kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza.
Majaliwa ametoa agizo hilo Oktoba 20, 2022 ofisini kwake jijini Dodoma wakati alipokutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR TAMISEMI) Angellah Kairuki pamoja na Viongozi wa Wilaya ya Ukerewe na Watendaji wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Amesema kampuni hiyo ilipewa kandarasi ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 13 kwa kiwango cha lami na changarawe katika kisiwa hicho ambapo ilipaswa kukamilisha kazi hiyo mwezi Julai mwaka huu.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, katika hili tumetoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa, tunachotegemea ni uaminifu wenu na utekelezaji wa miradi hii iwe ya viwango na mkamilishe kwa wakati”amesema Majaliwa
Aidha Majaliwa ameongeza kuwa ni vyema Mameneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Mikoa na Wilaya wakatekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuhakikisha ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali nchini na ukamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Angellah Kairuki amesema wamepokea maelekezo ya Waziri Mkuu na kuahidi kufanya mapitio makubwa ya mfumo wa kiutendaji wa TARURA ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ndani ya taasisi hiyo.




Discussion about this post