IBIDJAN,IVORY COAST
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameongoza majadiliano ya Tanzania na Wawekezaji mbalimbali wenye nia ya kuwekeza katika Mradi wa Umwagiliaji wa Bonde la Mara, majadiliano yaliofanyika katika Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika mwaka 2022 linalofanyika Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.
Akizungumza katika majadiliano hayo, Makamu wa Rais Dkt.Mpango amesema Tanzania ni sehemu sahihi zaidi ya uwekezaji kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuwa ni lango muhimu zaidi kibiashara kwa nchi za Afrika Mashariki zenye watu zaidi ya milioni 300 pamoja nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) zenye watu zaidi ya milioni 450.
Amesema uwepo wa ardhi ya kutosha na hali ya hewa inayofaa kwa kilimo kikubwa pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo inatoa ishara ya mazingira rafiki ya uwekezaji.
Dkt.Mpango amesema Tanzania ina hekta milioni 44 zilizoainishwa kwaajili ya kilimo, na takriban hekta milioni 10.8 pekee zinazolimwa. Ameongeza kwamba Eneo linalofaa kwa umwagiliaji linakadiriwa kuwa hekta milioni 29.4, na takriban asilimia 2.4 pekee zimetumika.
Pamoja na hayo, Makamu wa Rais ametaja juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan zenye lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji kama vile uboreshaji wa miundombinu ikiwemo reli na barabara, bandari, usafiri wa anga pamoja na maboresho katika upatikanaji wa nishati ya uhakika.
“Licha ya janga la Uviko 19 miradi ya uwekezaji kutoka mataifa ya nje iliosajiliwa nchini Tanzania imeongezeka mara tano zaidi hadi kufikia dola bilioni 2.2 mwaka 2021 kutoka dola milioni 454 mwaka 2020″amesema Dkt.Mpango
Awali akiwasilisha mradi huo kwa wawekezaji Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa amesema mradi huo unatarajia kuimarisha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, ufugaji na uvuvi pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo katika eneo hilo.
Aidha Mndolwa amesema mradi utaongeza kipato kwa wakulima wadogo wanaoishi maeneo hayo pamoja na kuongeza ajira na uzalishaji wenye tija.
Mradi wa Umwagiliaji wa Bonde la Mara unatarajiwa kutekelezwa katika wilaya ya Serengeti , Tarime na Butiama Mkoani Mara.




Discussion about this post