NA MWADISHI WETU,MWANZA
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameitaka menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuiwezesha kutimiza malengo yaliyowekwa.
Masanja ametoa kauli hiyo Desemba 19,2022 jijini Mwanza mara baada ya kuitembelea Menejimenti ya TAWA inayoendelea na mafunzo ya uongozi katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Pasiansi.
Masanja ameongeza kuwa utendaji kazi wenye kuzingatia ushirikiano na upendo ni nguzo muhimu itakayowawezesha kurekebishana na kukosoana kiutendaji kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Aidha, amesisitiza kuwa ni vyema menejimenti hiyo ikajiwekea utaratibu wa kujadili changamoto mbalimbali pamoja ili iweze kufika mbali kiutendaji.
“Mwenzako anapokutana na changamoto yoyote ichukulie kama ni yako,tunahitaji tufanikiwe kwa kutatua changamoto zinazotukabili kwa pamoja ” amesisitiza Masanja.
Mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo viongozi katika usimamizi wa masuala mbalimbali yakiwemo ya rasilimali watu, fedha na taratibu za manunuzi yametolewa kwa Manaibu Kamishna, Makamanda wa Kanda, Makamishna Wasaidizi Wandamizi na Makamishna Wasaidizi.




Discussion about this post