NA MWANDISHI WETU
SERIKALI inaendelea na jitihada za kutafuta vyanzo mbalimbali vya maji ili kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi wote.
Hata hivyo wakati Serikali inaendeelea na jitihada hizo,Wananchi wametakiwa pia kuwa na tabia ya kulinda na kutunza vyanzo vya maji pamoja na mazingira kwa kuwa kuharibu Mazingira ni kuhujumu.
Hayo yamezungumzwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Machi 16,2023 jijini Dar es Salaam mara baada ya kuzindua mradi wa kusambaza maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo uliotekelezwa na Serikali kwa ufadhili wa Benki ya Dunia ambao unategemea kunufaisha wananchi zaidi ya 450,000 kwa gharama ya Sh.Bilioni 70.
Majaliwa ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaa (DAWASA) kwa kutekeleza mradi kwa ufanisi na kwa wakati na kuongeza kuwa kukamilika kwa mradi kunatoa nafasi kwa wananchi kuanza kunufaika na maji ambapo utawanufaisha wakazi wa Tegeta A, Wazo, Goba,Madale na Mivumoni ambao wamekosa huduma ya maji kwa muda mrefu.
Amesema kuwa kwa sasa kazi iliyopo ni kuhakikisha wananchi wote wanafanyiwa maunganisho ya maji ili kila mmoja aone manufaa ya mradi huu nyumbani kwake.
“Serikali inatambua changamoto ya maji iliyokwepo kwenye maeneo haya, na ndio maana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alifanya uamuzi wa dhati wa kusukuma utekelezaji wa mradi huu ili wananchi mpate maji.
“Mameneja wa mikoa ya kihuduma DAWASA ongezeni nguvu katika kusambaza maji mitaani, nimepita kwenye kituo cha kusukuma maji na kwenye tenki, maji yanashuka yenyewe bila kusukumwa na umeme, hivyo hamna sababu ya kushindwa kusambaza maji kwa wananchi,” amesisitiza Majaliwa.
Katika hatua nyingine Majaliwa, amewataka wananchi kuwa makini na kutokukubali mtu yeyote kuwalaghai na kutaka rushwa kwa ajili ya kuunganishiwa maji, utaratibu wa Serikali wa kuunganisha watu maji uzingatiwe na kufuatwa ipasavyo.
“Niwatake wananchi kuwa na tabia ya kulinda na kutunza vyanzo vya maji pamoja na mazingira, kuharibu Mazingira ni kuhujumu.
“Serikali kwa pamoja inaendelea na jitihada mbalimbali za kutafuta vyanzo mbalimbali vya maji ili kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote,” amefafanua Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kuzindua rasmi maadhimisho ya wiki ya maji Duniani inayoanza Machi 16 hadi 22,2023
Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameipongeza DAWASA kwa kufanikisha utekelezwaji wa mradi mkubwa uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu na kuongeza kuwa kazi ya kufanya sasa ni kuharakisha wananchi wanapata maji.
“Pasiwepo na usumbufu katika kuwaunganisha wananchi na huduma ya maji, ndani ya siku 14 za kazi mwananchi aliyekidhi vigezo apewa huduma ndani ya muda,” ameeleza Aweso.
Hata hivyo Aweso amefafanuwa kuwa kuwa rasilimali zilizopo nchini ni toshelevu kuweza kutoa huduma kwa wananchi wote, hivyo pasiwepo na usumbufu katika kutoa huduma.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaa(DAWASA) Kiula Kingu amesema kuwa mradi huu umetekelezwa kikamilifu ukihusisha ujenzi wa matenki makubwa matatu ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita milioni tano kila moja, ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji, ulazaji wa bomba kubwa la nchi 16 ambalo litasafirisha maji kwa umbali wa kilomita 1,252.
Mkazi wa Tegeta A Mwanahija Hassan ameishukuru Serikali kwa jitihada zilizofanyika za kufikisha maji katika maneno yao kwa kuwa amekuwa wakitumia maji ya kununua kwa gharama kubwa na yenye chumbi kwa miaka mingi.




Discussion about this post