NA MWANDISHI WETU,DODOMA
WAKUU wa Wilaya nchini kuweka ajenda ya mazingira kama kipaumbele katika maeneo yao ikiwemo kubuni mikakati endelevu ya kupunguza matumizi ya mkaa na kuni ili kasi ya ukataji wa miti kwa ajili ya kupata nishati hiyo ya kupikia iweze kupungua.
Wito huo umetolewa Machi 17,2023 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo wakati akiwasilisha vipaumbele vya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa wakuu wa wilaya ili kuwajengea uelewa utakaowasaidia kusimamia utekelezaji wa vipaumbele vinavyotekelezwa katika maeneo yao ya utawala.
Dkt.Jafo ametoa wito huo wakati wa semina elekezi kwa wakuu wa wilaya iliyozinduliwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango inayofanyika jijini Dodoma ambapo amewataka pia kuendelea kusimamia vyema zoezi la upandaji wa miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri.
Aidha, Dkt. Jafo amewapongeza viongozi hao kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha kuwa mazingira yanahifadhiwa kwa kusimamia vyema zoezi la upandaji miti.
“Ndugu zangu tangu tuzindue Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira mwaka 2021, ninyi wakuu wa wilaya mmekuwa mkisimamia ipasavyo kampeni hii kwa kuhamasisha upandaji wa miti, mmemuheshimisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Dkt.Jafo .
Hata hivyo amewasihi viongozi hao kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji ili kuepuka changamoto ya kukauka kwa vyanzo hivyo hali inayoweza kusababisha uhaba wa maji kama ambavyo uliikumba nchi yetu katika baadhi ya maeneo hivi karibuni.
Hatua ya wizara kuwasilisha vipaumbele hivyo ni kunatokana na maombi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR- TAMISEMI) ya kutaka wakuu hao kupitishwa kwenye utekelezaji wa shughuli za wizara za kisekta ili kwenda kusimamia na kutekeleza majukumu hayo kwa weledi.
Lengo la uwezeshaji huo ni kuwajengea uwezo viongozi hao ngazi ya wilaya ili kuwawezesha kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa weledi na kuelewa mipaka na miongozo ya kusimamia wakati wanatekeleza majukumu yao.




Discussion about this post