NA GOODLUCK HONGO
MRATIBU wa Uhaulishaji Teknolojia na Mahusiano kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kituo Cha Mikocheni jijini Dar es Salaam Vidah Mahava amesema mahitaji ya zao la Nazi kwa sasa ni makubwa kuliko inavyodhaniwa.
Mahava amesema hata wale wenye viwanda vinavyotumia zao hilo kuzalisha bidhaa bado wanaagiza kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji yao.
Kauli ya Mahava imekuja wakati ambapo Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ikiendelea kumuwezesha Mtafiti na Mbunifu Tiberius Mario aliyebuni Kaboni inayotokana na vifuu vya nazi ili itumike kama mbadala wa kemikali hatari ya Zebaki inayotumiwa na wachumbaji wadogo katika kuchenjulia dhahabu.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni wa wiki jijini Dar es Salaam waliotembelea Kituo hicho kujifunza teknolojia ya uzalishaji wa miche kwa njia ya Chupa(Tissue Culture),Mahava amesema mara nyingi wamekuwa wakiwaambia wadau wa zao hilo kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo na kutumia miche yao ambayo wameifanyia utafiti na kuipatia huduma bora ili iweze kuzaa zaidi.
Amesema kwa sasa nazi ina mahitaji mengi na zinahitajika sana kutokana na matumizi yake hivyo bado hatujaweza kukidhi mahitaji hayo.
“Naomba niwaambie kwamba hata nazi mnazoziona watu wanazozipikia bado mahitaji ni makubwa na zile zinazotumika viwandani nyingine zinaagizwa kutoka nje ya nchi”amesema Mahava
Amesema Kituo chao cha TARI-Mikocheni ni moja kati ya Vituo 17 vinavyofanya Utafiti wa Kilimo ambapo pamoja na mazao mengine lakini wao pia wamejikita zaidi katika kuendeleza zao la Minazi na kusimamia masuala yote ya bayoteknolojia.
“Minazi inaanza kuzaa kuanzia miaka mitano hadi saba na hii ndio minazi tuliyonayo lakini hapa katikati iliwahi kuletwa minazi inayoanza kuzaa miaka mitatu ni sawa lakini bado ilionekana haifanyi vizuri sana na inaonekana ikizaa baada ya muda mfupi inakufa kutokana na magonjwa lakini pia haikuweza kustahimili hali ya hewa.
“Lakini minazi ambayo tumefanyia utafiti na ambayo tunasambaza sasa ni hii minazi ya asili inayoitwa East African Tall ambayo inaanza kuzaa baada ya miaka mitano hadi saba na inaweza kuzaa hadi nazi 70 na kuendelea lakini pia tunaendelea kufanyia utafiti zaidi ili iweze kuzaa nazi nyingi zaidi zinazofikia 100 na kuendelea.
“Minazi mingi iliyopo ni ile ambayo wamepanda siku nyingi sana hivyo kauli yetu mara nyingi tumekuwa tukiwaambia wadau kwamba sasa waanze kupanda minazi mipya na ile iliyopo wailime kwa kufuata Kanuni Bora za Kilimo lakini pia mingi iliyopo ukiangalia kwa haraka haihudumiwi”amebainisha Mahava
Kwa upande wake Mtafiti kutoka Kituo hicho Chona Mahushi amesema lengo la Utafiti ni kutatua changamoto za masuala ya kilimo kwa wakulima hivyo minazi mirefu ambayo wao ndio wanayoifanyia utafiti ndio bora zaidi kwa kuwa inakaa muda mrefu na inahimili magonjwa mbalimbali.
Hata hivyo wakulima wa zao hilo na wengine wameombwa kufika katika vituo hivyo vya utafiti vilivyo katika kila eneo nchini ili waweze kupata ufumbuzi wa matatizo yao ya kilimo kulingana na mazao wanayozalisha ili wafaidike na kilimo chao.
Awali akizungumza Machi 8,2023 mbele ya waandishi wa habari na watafiti jijini Dar es Salaam wakati wa Mafunzo ya Uandishi wa Habari za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu kati ya waandishi wa habari na watafiti yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),Mario amesema Tanzania inauwezo wa kuokoa dola za kimarekani Milioni sita za kuagiza Kaboni kutoka nje ya nchi.
Amesema Tanzania ni nchi ya 16 duniani kwa kuzalisha nazi baada ya nchi kama Indonesia,India,Brazil na Ufilipino lakini pia ni fursa pia kwa watanzania kujua kuwa vifuu vya nazi ni mali inayoweza kuzalisha Kaboni.
“Baada ya kumaliza Chuo nilianza kufanya utafiti wa kuzalisha Kaboni na ndipo nilipobuni uzalishaji kwa kutumia vifuu vya nazi na baada ya kupimwa na kuthibitishwa imeonekana kuwa na uwezo wa asilimia 98 kukamata madini yaliyopo katika udongo”amesema Mario
Amesema kila mgodi wa dhababu lazima uwe na Kaboni kwa ajili ya kusaidia kukamatisha dhababu na Tanzania inahitaji tani 1500 pekee za Kaboni ambazo asilimia kubwa huingizwa kutoka nje ya nchi.
Mario ameongeza kuwa pamoja na yeye kufanikiwa kuzalisha Kaboni kwa kutumia vifuu vya nazi ambapo baadhi ya maeneo katika jijini la Dar es Salaam tayari wameshazoea kumuuzia lakini gharama za uzalishaji ni kubwa.
Kilimo cha Minazi sasa kimeanza kuonekana kama ni fursa zaidi ambapo faida zake ni pamoja kuzalisha mbao ambazo zinatengeneza vitu mbalimbali ikiwemo dhamani za ofisini,nyumbani na hata wakati mwngine kutumika mihimi ya madaraja ya asili,kuzalisha nazi zinazotumika kama kiungo katika mboga,mafuta ambayo watu hujipaka mwilimi,ufagio maarufu kama fagio la chelewa.




Discussion about this post