NA GOODLUCK HONGO
JANUARI 12,2023,Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Atomiki, (IAEA) lilitoa taarifa juu ya kupandwa kwa mbegu za mazao mbalimbali ya kilimo katika kituo cha anga za juu.
Mbegu hizo zilipelekwa mwezi Novemba mwaka 2022 na zilipandwa kama sehemu ya utafiti wa kuimarisha aina mbalimbali za mbegu zinazohimili mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya IAEA inaeleza kuwa tayari mbegu hizo ikiwemo Mtama zimepandwa eneo la ndani na nje ya kituo hicho na hivyo zinapata miali kamilifu ya anga za juu pamoja na viwango vya juu zaidi vya joto kwenye eneo hilo.
Kwa mujibu wa IAEA yenye Makao yake Makuu, Vienna nchini Australia, mbegu hizo zilipelekwa na shirika hilo pamoja na lile la Chakula na Kilimo Duniani(FAO) kwa lengo la kuchunguza athari za miali ya anga za juu kwenye mbegu kama sehemu ya utafiti wa kuimarisha aina mbalimbali za mbegu zinazohimili mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuongeza uhakika wa chakula.
“Lengo ni kubaini iwapo mazingira magumu ya hali ya hewa anga za juu kama vile joto kali kupindukia, miale kutoka anga za juu vinaweza kuchochea mabadiliko kwenye mbegu na hatimaye mabadiliko hayo ya hali ya hewa yanaweza kusaidia mimea kuwa na mnepo zaidi pindi inapokabiliwa na changamoto za ukuaji au kumea duniani,” inaeleza taarifa hiyo.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IAEA ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Nyuklia na Matumizi yake, Najat Mokhtar anasema wana wajibu wa kuchunguza teknolojia za kinyuklia ambazo zinaweza kuleta tofauti chanya kwa afya ya binadamu na chakula anachokula.
“Jinsi dunia inahaha kuhimili madhara ya mabadiliko ya tabianchi, tunahitaji kuongeza kasi ya tafiti za kuboresha mimea na kupata majawabu yanayotesheleza na fanisi,” anasema Mokthar.
Kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa Dunia imeanza kuona mazingira tofauti ya uzalisha wa chakula kutoka na ardhi kushindwa kuhimili mazingira yake baada ya uhabiribifu wa mazingira unaosababisha athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo Dunia inaelekea kuwa sehemu isiyo salama ya kuishi kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ambapo kusambaa kwa silaha za nyuklia kunaendelea kuhatarisha uhai wa binadamu na mazingira yake.
Tayari Japan imeshaonja madhara ya mabomu ya atomiki miaka zaidi ya 50 iliyopita baada ya Marekani kuyaangusha katika miji ya Nagasaki na Hiroshima ili kushinda vita.
Wakati athari hizo zikiendelea Dunia imeendelea kukumbwa na migogoro katika kila maeneo mbalimbali kutokana kusambaa kwa silaha mikononi mwa raia na uwepo wa makundi ya wanamgambo ambao wanatishia mazingira ya kilimo kwa wakulima ili kuzalisha chakula.
Hata hivyo wanasayansi wameanza kujikita na uzalishaji wa vyakula kwa njia ya maabara zikiwemo mbegu za mazao mbalimbali ya chakula ili kuimarisha usalama wa chakula na upatikanaji wake.
Kwa sasa kumekuwa na mjadala katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki juu ya matumizi ya mbegu za mahindi yaliyokuzwa maabara maarufu kama GMO.
GMO ni mazao yenye vinasaba vilivyoundwa baada ya mbegu kufanyiwa uhandisi jeni ambapo inadaiwa kuwa mazao yaliyoundwa na vinasaba vilivyofanyiwa uhandisi jeni yanatajwa kuwa na athari kwa viumbe hai wakiwamo binadamu, wanyama hata mazingira.
Mbegu hizo za GMO zinadaiwa kuongezwa vinasaba ili ziweze kutoa mazao mengi na kwa muda mfupi tofauti na mbegu za asili ambazo hukua kulingana na mazingira yake ya asili.
Baadhi ya wataalamu wanaeleza kuwa mbegu za mahindi ya GMO haziwezi kupandwa tena baada ya mazao yake kuvunwa na hata zikipandwa hazioti.
Kutokana na hali hiyo Kenya iliingia katika mzozo wa mahindi ya GMO baada ya Serikali ya nchi hiyo kuruhusu kuingizwa nchini humo tani zaidi ya milioni 10 za mahindi hayo yaliyokuzwa kisayansi ili kusaidia katika maeneo yaliyokumbwa na uhaba wa chakula.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wabunge wa nchi hiyo kupinga kuingizwa kwa chakula hicho lakini walishangaa kuona meli yenye mzigo huo ikiwa imetia nanga bandarini.
Wakati Kenya ikiendelea na mzozo juu ya GMO,Serikali ya Tanzania iliweka wazi msimamo wake juu ya suala hilo.
Msimamo huo wa Serikali umewekwa wazi na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe jijini Dodoma Januari 10,2022 wakati akizungumza na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
Bashe anasema mbegu za pamba za GMO zinazotumiwa na baadhi ya nchi jirani huzalisha nusu ya pamba inayozalishwa kwa kila ekari moja inayovunwa Tanzania kwa kutumia mbegu bora za asili zilizofanyiwa utafiti na watanzania.
Hata hivyo Waziri Bashe anaongeza kuwa wizara itaendeleza tafiti za mbegu ili kuzalisha mbegu bora jambo linaonyesha mafanikio makubwa katika matumizi yake.
“Kwa sasa Tanzania haipo tayari kutumia mbegu zilizofanyiwa mabadiliko ya vinasaba lakini itajenga maabara mbili kwa ajili ya kuendelea kujifunza ili kuliepusha taifa kutumia wasichokijua”anasema Bashe
Akizungumza katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine mkoani Morogoro, Bashe anafafanua kuwa Rais ametoa fedha za utafiti na sasa zimeongezeka mwaka huu wa fedha kiasi cha Sh.Bilioni 84 kutoka Bilioni 15.
“Nimewaagiza TARI(Taasisi ya Utafiti wa Kilimo) sisi hatutumii GMO lakini hatuwezi kukataa kuijua GMO,tumetenga vituo ndani ya Wizara ya Kilimo viwili kwa maana (MARI) yaani Mikocheni Research Istitute na kingine cha Makutupora kwamba hivi vituo viwili ndio vitakuwa centre of excellency by technologies pratices kwa kushirikiana na Sokoine University.”anasema Bashe
Aidha anabainisha kuwa ni lazima waijue GMO na hawawezi kujua miaka 20 ijayo dunia ikawalazimisha kuwa hawawezi kuendelea bila kuwa na GMO ambapo hapo ndipo inawezekana kutumia GMO ya kwao badala ya kwenu.
“Wanafunzi wanasoma,wanamaliza na wanakuja mtaani sasa hatuwezi kuikataa hii sayansi”amesema Bashe
Tayari baadhi ya nchi kama Malaysia zimeanza kuruhusu mbegu za GMO za zao la ngano kuzalishwa nchini humo.
Hata hivyo TARI kituo cha Mikocheni jijini Dar es Salaam kinaendelea na tafiti za mbegu bora ambapo inatarajiwa kuzalisha miche 500,000 ya zao la Mkonge kwa kutumia teknolojia ya chupa maarufu kama (Tissue culture)kutokana na ongezeko la mahitaji yake kitaifa.
Mbali na hilo lakini pia taasisi hiyo inaendelea na uzalisha wa miche bora ya zao la Nanasi ambalo hukaa muda mrefu bila kuharibika na lenye ubora wa kuuzwa nje ya nchi bila tatizo.
Machi 7,2023 Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) chini ya Mkurugenzi wake Dk.Amos Nungu imekuwa ikihimiza waandishi wa habari kujikita katika kuandika habari za Sayansi,Teknolojia na Utafiti ili kusaidia jamii kutatua changamoto zinazowakabili kwa kujua tafiti,teknolojia ambazo serikali imekuwa ikiwekeza ili kuwa na Taifa linalojitegemea kwa teknolojia yake.
Hata hivyo COSTECH iliandaa Mafunzo ya Uandishi wa Habari za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu kati ya waandishi wa Habari na Watafiti.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mratibu wa Mafunzo ya Uandishi wa Habari za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu kutoka Tume hiyo Deusideth Leoanaed anasema hayo ni mafunzo ya tisa kufanyika tangu mwaka 2015 ya kuwakutanisha Waandishi wa Habari,Watafiti na Wabunifu.
“Lengo ni kuwaleta pamoja na kubadilishana uzoefu ili tafiti nyingi ziweze kuandikwa kwa lugha rahisi,kupata ongezeko la uhawilishaji wa teknolojia kati ya Watafiti na Jamii na kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kuandika taarifa za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu kama ilivyo katika maeneo mengine ikiwemo siasa na michezo”anasema Leonaed.




Discussion about this post