NA MBARAKA KAMBONA,SINGIDA
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Sh. Milioni 878. 4 kwa ajili ya kununua madume bora 366 ya ng’ombe ili wafugaji waweze kuboresha mifugo yao.
Madume hayo yatawawezesha wafugaji kuwa na ng’ombe chotara ambao wanauwezo wa kuzalisha wastani wa kilo 150- 200 za nyama ukilinganisha na uzalishaji wa kilo 80-120 kwa Ng’ombe wa asili
Hayo yamezungumzwa Aprili 6,2023 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega wakati wa hafla ya kugawa madume bora 40 kwa vikundi vya wafugaji iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida.
Amesema ni kwa wafugaji kujua kuwa soko la nyama inayozalishwa hapa nchini limefunguka hivyo wajipange kubadilika na kufanya ufugaji wa kibiashara ili waweze kuongeza tija katika uzalishaji.
“Ndio maana Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Sh. Milioni 878. 4 kwa ajili ya kununua haya madume bora 366 ili wafugaji tuweze kuboresha mifugo yetu, tuweze kupata ng’ombe wanaoweza kutoa nyama nyingi na kufanya biashara yenye tija kuliko hivi sasa.
“Mifugo ni uchumi, na leo nawaambieni nyama ni dili, Rais Samia amefungua milango, wakati huu tunapokea wageni wengi kutoka nje ya nchi wakitaka kufanya biashara ya nyama na nchi yetu”amesema Ulega
Naye, Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga amemshukuru Waziri Ulega kwa kuwezesha wafugaji wa Wilaya ya Mkalama kupata madume bora 40 na kuahidi kuyatumia vizuri madume hayo kuboresha uzalishaji wa mifugo yao.
Halmashauri ambazo zimepata mgao huo ni pamoja na Mkuranga 50, Mvomero 40, Buchosa 46, Chamwino 50, Maswa 50, Chato 50, Msalala 50 na Mkalama 40.




Discussion about this post