NA GOODLUCK HONGO
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amependekeza kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)kupitia Wizara ya Nishati na Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka mpango mkakati wa kurudisha vyura wa Kihansi ili kuepuka gharama kwa Shirika la Umeme Tanzania.
Amesema malipo ya kutunza Vyura wa Kihansi katika bustani ya wanyamaya Marekani ni Sh. Milioni 612 AMBAPO mwaka 2000 Tanzania ilisafirisha vyura 500 kwenda bustani ya wanyama ya Bronx na Toledo iliyopo Marekani ili kuepuka hatari ya kupotea kwa vyura ambayo ilitokana na utekelezaji wa mradi wa umeme wa maji wa Kihansi mnamo mwaka 1994.
CAG Kichere ameeleza hayo katika Ripoti yake ya Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mashirika ya Umma kwa wa fedha 2021/2022 iliyotolewa Machi 29,2023
Amesema ingawa haiwezekani kubainisha idadi kamili ya sasa ya vyura vinavyosimamiwa nchini Marekani, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linagharamia dola za Marekani 130,000 kwa mwaka kwa ajili ya kutunza vyura hao, ambapo inakadiriwa takribani ya dola za Marekani milioni 2.86 zilitumika kwa miaka yote 22 ya kuhudumia vyura.
“Katika mwaka 2020/21 na 2021/22 ilifanya malipo ya shilingi milioni 611.92 (sawa na dola za Marekani 260,000).
“Nimebaini kuwa mkataba kati ya Tanzania na bustani za wanyama za Marekani ulimalizika mnamo Juni 2020 na kuongezewa muda wa miaka miwili hadi Juni 2022,japokuwa hakukuwa na mpango
wowote wa kurudisha vyura hao Tanzania ikizingatiwa kuwa tayari miaka 22 imepita tangu vyura 500 wapelekwe kwenye bustani za wanyama za huko Marekani.
“Ninapendekeza Shirika la Umeme Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Wizara ya Maliasili na Utalii iweke mpango mkakati wa kurudisha vyura wa Kihansi ili kuepuka gharama kwa
Shirika la Umeme Tanzania.”amesema CAG Kichere
Awali Vyura wa Kihansi ambao kitaalamu wanaitwa nectophrynoides asperginis ni ambao ni maarufu kwa kuzaa wanatajwa katika orodha ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanyama na Mimea iliyo hatarini kutoweka (Cites), na kuwafanya wanalindwe kisheria na ni marufuku kuwauza sehemu yoyote duniani.
Tofauti na vyura wa kawaida ambao hutaga mayai na kuyaacha majini yakielea katika utando na kisha huanguliwa wakati unapowadia, lakini wa Kihansi huangulia tumboni.
Vyura hao waligungulika katika Mto Kihansi ambao unafanya maporomoko katika milima ya Udzungwa unaoanzia Mufindi na Kilolo mkoani Iringa na kumwaga maji yake katika Bonde la Kilombero Mkoa wa Morogoro ambapo mradi wa umeme wa megawati 180 ulizinduliwa katika maporomoko ya mto huo.




Discussion about this post