NA MWANDISHI WETU
MTAFITI na Mbunifu wa Kaboni inayotokana na vifuu vya nazi Tiberius Mario amesema kwa sasa ameomba fedha kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ili aweze kufanya utafiti juu ya kaboni yake kutumika katika kilimo.
Hayo ameyasema Aprili 9,2023 wakati akizungumza na Bajeti juu ya matumizi ya Kaboni hiyo kutumika kuondoa sumu iliyopo katika ardhi inayotumika kwa kilimo ama itakuwa na madhara ikiwa itatumika au itasaidia.
Amesema Kaboni anayotengeneza ina uwezo wa kutumika kusafisha maji kwa kunyonya uchafu lakini pia kwa watumiaji wadogo wa dhahabu katika eneo la uchenjuaji madini hayo hivyo kutokana na hilo ameona ni muhimu kufanya utafiti katika suala zima la kilimo ikiwa inamadhara au inasaidia
“Kwa sasa hatuwezi kusema kama inafaida katika ardhi ya kilimo am hasara hadi tufanye utafiti wa kina na kujiridhisha ndio sasa tutoe matokeo na kuona nini cha kufanya lakini sasa bado.
“Tumetuma maombi kwa WFP lakini bado hawajatujibu na tunaendelea kusubiri ili tufanye utafiti ambao Kaboni yetu inaweza kutumika katika ardhi ya kilimo kwa kunyonya sumu ili mazao yaweze kukuwa katika ardhi yenye virutubisho ama itakuwa na madhara katika ukuaji wa mimea”amesema Mario.
Mario ambaye ni mshindi kwa kwanza katika Mashindano ya Sayansi na Teknolojia maarufu kama (MAKISATU) yanayoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) mwaka 2022 amesema Kaboni yake imethibitishwa kwa asilimia 98 kufanya kazi inayotakiwa.
Aidha ameongeza kuwa kwa sasa baadhi ya makampuni makubwa ya uchimbaji dhahabu wameanza kuitumia Kaboni aliyoibuni kwa kutumia vifuu vya nazi katika kukamatishia madini ya hadhabu na wamethibitisha kuwa inafanya kazi nzuri.
Hata hivyo Mario amesema licha ya kusaidiwa na COSTECH kufika hapo alipofika lakini anahitaji kiasi cha Sh.Milioni 36 kufanikisha ndoto yake na kuwa na kiwanda kikubwa chenye uwezo wa kuzalisha maelfu ya tani za Kaboni ili zisiagizwe kutoka nje ya nchi.




Discussion about this post