NA GOODLUCK HONGO
BIASHARA haramu ya Viumbe na Mimea pori (Wildlife) imetajwa kushika nafasi ya nne duniani baada ya ile ya binadamu,dawa za kulevya na bidhaa feki ambapo imefikia kiasi cha dola za kimarekani Bilioni 23.
Hayo yameelezwa Mei 26,2023 jijini Dar es Salaam na Mtaalamu wa Masuala ya Wanyamapori kutoka jijini Arusha Allen Mgaza wakati wa semina kwa waandishi wa habari juu ya uhalifu dhidi ya wanyamapori iliyoandaliwa na Taasisi ya Infonile kutoka nchini Uganda.
Akizungumzia biashara hiyo,Mgaza amesema biashara hiyo ni tishio kwa Taifa na kimataifa hivyo kunahitajika juhudi kubwa kwa kushirikiana na serikali ili kupambana na biashara hiyo ya viumbe pori licha ya kuwa baadhi ya biashara hiyo inafanywa kihalali.
Amesema wafanyabishara haramu wa viumbe na mimea pori hutumia njia mbalimbali za kificho katika kusafirisha malighafi hizo ili wasiweze kugundulika
“Masuala ya tibaasili yanachangia kuwepo kwa biashara hiyo kutokana na kuwepo kwa mimea inayovunwa kwa ajili ya dawa.
“Kuna ndege aina ya Tumbusi ambao wao hula mizoga ya wanyamapori hivyo kuna watu wanaimani kuwa wakipata kichwa cha ndege huyo basi watafanikiwa zaidi hivyo kufanya kila jitihada ili kuwauwa na kuchukua vichwa vyao.
“Sababu nyingine ya kuwepo kwa biashara hiyo ni kutumika kama chakula,kutengeneza vipodozi,kukamata wanyama kwa ajili ya kuwafunga binafsi na mwisho ni sababu za kisayansi”amesema Mgaza
Aidha ameongeza kuwa fedha zinazopatikana kutokana biashara hiyo zinadaiwa kutumika katika kufadhili makundi ya kigaidi,kuongeza rushwa na wakati mwingine ni hatari kwa kusababisha magonjwa yanayouwa watu wengi kama ebola na mafua ya ndege.
“Kuna umuhimu mkubwa wa kupambana na biashara hii hatari ambapo ikiwa haitadhibitiwa basi vizazi vijavyo havitaweza kuwaona tena wanyama na mimea pori”amesema Mgaza
Kwa upande wake Mwakilishi wa Taasisi ya Infonile nchini Daniel Samson amebainisha kuwa waandishi wa habari wanaweza kusaidia katika kukabiliana na biashara hiyo kwa kufichua na kuandika habari na mazingira yanayopeleka uwepo wake
“Waandishi wa habari waendelee kutumia zana kama WILDEYE katika kuwasaidia kupata taarifa za uhalifu dhidi ya wanyamapori nchini na nje ya nchi ndio maana Infoline iliamua kuandaa warsha ya kuwakutanisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali ili kuwajengea uwezo juu ya uhalifu dhidi ya wanyamapori na faida zake ikiwa watalindwa”amesema Samson




Discussion about this post