NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,amewasihi wasomi nchini kufanya utafiti wa kina wa kufuatilia na kutathmini kitaalamu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ili wananchi wajue mafanikio hayo.
Mbeto ametoa kauli hiyo Juni 16,2023 Visiwani Zanzibar katika kongamano la kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi, la kuelekea miaka mitatu ya uongozi wake ambalo liliandaliwa na Tawi la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kusini Unguja.
Ameeleza kuwa utafiti huo utawasaidia wananchi kuepuka upotoshaji unaofanywa kwa sasa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kupitia mikutano yao ya hadhara iliyofanyika kisiwani Pemba.
Mbeto, ameongeza kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa za kimaendeleo chini ya uongozi wa Dk.Mwinyi,hivyo wanasiasa na viongozi wa upinzani wanatakiwa kuthamini na kuunga mkono juhudi hizo badala ya kubeza na kupuuza kwani nao ni miongoni mwa wanufaika wa maendeleo hayo.
“Wasomi msikubali kudanganywa fanyeni utafiti juu ya kazi kubwa iliyofanywa na Dk.Mwinyi toka aingie madarakani mpaka sasa, leteni majibu na kuibua hoja makini za kujenga mshikamano na maridhiano ya kisiasa yanayohimiza ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Wapinzani tunajua hawawezi kumpongeza wala kusifu juhudi hizo lakini japo mthamini na kuheshimu mamlaka za kiutawala,kwani nanyi ni wananufaika juu ya maendeleo hayo kwani ruzuku,mishahara na huduma zote muhimu za kibinadamu zinazofanywa na Serikali nanyi mnapata kama wananchi wengine”,amesema Mbeto.
Mbeto,amebainisha kuwa Serikali ya awamu ya nane chini ya Uongozi wa Dk.Hussein Ali Mwinyi, inatekeleza kwa ufanisi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 katika sekta mbalimbali nchini.
“Miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk.Mwinyi, tayari amejenga Shule za kisasa kuanzia ngazi za msingi hadi Vyuo Vikuu ili vijana wasome katika mazingira rafiki yanayoendana na mahitaji ya kitaaluma.
“Katika kuimarisha Uchumi wa nchi serikali imefungua milango ya uwekezaji kwa kusajili miradi mbalimbali ya maendeleo itakayojenga mahoteli makubwa ya kitalii ikiwemo kuimarisha sekta mbalimbali za miundombinu,Afya,Elimu, Anga,Nchi kavu na baharini,Utalii,Uwezeshaji Wananchi kiuchumi,Ustawi wa Jamii na kuweka Mazingira rafiki katika Uchumi wa buluu”amebainisha Mbeto
Mbeto, amewasihi wananchi wasikubali kupotoshwa kwani nchi ipo salama na inapiga hatua kubwa katika nyanja za kiuchumi,kijamii,kisiasa,kiutamaduni na michezo nan kasi ya utendaji wa Serikali hiyo ya awamu ya nane imekuwa ni tishio kwa vyama vya upinzani nchini hali inayosababisha waanze kuchanganyikiwa na kutoa hoja dhaifu.




Discussion about this post