NA MWANDISHI WETU
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG Charles Kichere amesema Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) linalipa gharama zaidi za fedha za kigeni kwa kuhudhuria mikutano Kisumu, nchini Kenya juu ya Mradi wa Kituo cha Utafutaji na Uokoaji cha Ziwa Viktoria unaotekelezwa na nchi za Uganda na Tanzania pekee.
Aidha amebaini kuwa kufanyika kwa shughuli za mradi mbali na nchi washirika kunaweza kuchelewesha utekelezaji wake
Kwa mujibu wa Taarifa Kuu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mwaka 2021/22 kuhusu Miradi ya Maendeleo iliyotolewa Machi 29,2023 na CAG Kichere ambapo amesema Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkutanowake wa kawaida wa 14 uliofanyika Septemba 4,2009, lilikubali ujenzi wa Kituo cha Utafutaji na Uokoaji cha Ziwa Viktoria (MRCC) katika mkoa wa Mwanza.
Amesema Mradi huo unatekelezwa na nchi ya Uganda na Tanzania tu ambapo amebaini kuwa ujenzi wa Kituo hicho haukutekelezwa hadi kufikia October 25, 2022 hivyo mikutano inayoandaliwa na Tume ya Bonde la Ziwa Viktoria (LVBC) imekuwa ikifanyikia Kisumu, nchini Kenya.
CAG Kichere amebainisha kuwa mradi huo kupitia Tume ya Bonde la Ziwa Viktoria umemwajiri Mratibu wa Mradi wa kikanda tangu mwaka 2020 ambaye amekuwa akifanya kazi akitokea Kisumu, nchini Kenya kinyume na masharti ya mkataba wa ajira Na: LVBC/AFDB/IC/01/2021/22, ambao unaeleza kuwa kituo chake cha kazi ni mkoani Mwanza nchini Tanzania.
“Kwa hivyo, TASAC inalipa gharama zaidi za fedha za kigeni kwa kuhudhuria mikutano Kisumu, nchini Kenya na kwa upande mwingine, kufanyika kwa shughuli za mradi mbali na nchi washirika kunaweza kuchelewesha utekelezaji wake.
“Ninapendekeza TASAC ihakikishe Ofisi za Tume ya Bonde la Ziwa Viktoria (LVBC na Tume pamoja na mratibu wa mradi vinahamia kwenye eneo la mradi kwa utekelezaji wa haraka wa mradi wa MLVMCT,pia iharakishe ujenzi wa Kituo cha Utafutaji na Uokoajicha Ziwa Viktoria mkoani Mwanza”amesema CAG Kichere
Wakati huo huo CAG Kichere ameeleza kuwa katika ukaguzi wake wa mradi wa Kimataifa wa Usafiri na Mawasiliano wa Ziwa Viktoria (MLVMCT) unaotekelezwa na TASAC ulibaini kuwa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika Mkutano wa kawada wa 14 uliofanyika Septemba 4,2009, uliidhinisha ujenzi wa Kituo cha Utafutaji na Uokoaji cha Ziwa Victoria (MRCC) katika mkoa wa Mwanza.
“Nilibaini kuwa,muda wa utekelezaji wa mradi huu ulikuwa wa miaka minne kuanzia Mei, 2018 hadi Mei, 2022 na washirka wa mradi huu walipaswa kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) itakayosimamia utekelezaji wa shughuli za mradi za kikanda.
“Hata hivyo, nilibaini kuwa hadi Novemba 2022 rasimu ya Hati ya Makubaliano kati ya Tanzania na Uganda haikuidhinishwa licha ya Tume ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) kubaki mtekelezaji wa mradi huo”ameeleza CAG Kichere
Ameongeza kuwa hali hiyo imesababishwa na mchakato mrefu wa uhakiki wa rasimu ya Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya nchi washirika, kuhusiana na hili, malengo yaliyokusudiwa ya mradi hayakufikiwa kama inavyotarajiwa kwani imepelekea kuongezwa kwa muda wa utekelezaji wa mradi kutoka Mei 2022 hadi Aprili 2023.
“Ninapendekeza Serikali ya Tanzania na Uganda kuharakisha uhakiki wa rasimu ya Hati ya Makubaliano ili uidhinishwe kwa ajili ya utekelezaji bora wa mradi huu”amefafanua CAG Kichere




Discussion about this post