WARSAW,POLAND
MAMLAKA ya mifugo nchini Poland inachunguza ugonjwa wa ajabu unaoua pakana kuwataka wamiliki wa viumbe hao kuwafungia ndani ili kuepuka kusambaa zaidi.
Kwa mujibu wa tovuti ya RT News ambayo ilinukuu vyombo vya habari vya Poland Juni 28,2023 imeeleza kuwa idadi kubwa ya paka wameugua ugonjwa usioeleweka katika wiki chache zilizopita kote nchini Poland huku wengine wakifa kutokana na ugonjwa wa kushangaza kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Poland vilivyoripoti ugonjwa huo.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa kituo cha habari cha Notes From Poland imeeleza kuwa uchunguzi wa awali umegundua kuwa baadhi ya Paka waliokufa walikuwa wameambukizwa homa ya ndege.
Inasemekana kwamba Paka walioathirika na ugonjwa huo walipata dalili za mishipa ya fahamu na kupumua, ikiwa ni pamoja na homa kali, kukosa hamu ya kula na kukosa pumzi.
Wataalamu wanaamini kuwa dalili hizo zinaashiria aina fulani ya ugonjwa wa kuambukiza unaoenea kote nchini humo.
Mkurugenzi wa Kliniki ya Mifugo ya Tri-City huko Gdansk kaskazini mwa Poland, Paulina Grzelakowska ameema kuwa ugonjwa huo una mwanzo wa ghafla na unaendelea kwa kasi.
“Wanyama hao hufa kwa muda mfupi,” aliiambia TVN24, akibainisha kuwa paka wa rika zote wameathiriwa, bila kujali kama waliwekwa ndani au nje au walikuwa wamechanjwa dhidi ya magonjwa ya kuambukiza.
Wakati huo huo, Ofisi Kuu ya Mifugo ya Mkoa wa Pomerania nchini humo imeripoti kwamba, kati ya paka 28 walioletwa kliniki katika eneo la Gdansk katika wiki mbili zilizopita wakiwa na dalili kama hizo, 25 wamekufa.
Ukaguzi wa Kitaifa wa mifugo umebaini kuwa kati ya paka 11 ambao hadi sasa wamejaribiwa kote nchini humo tisa wamethibitika kuwa na virusi vya mafua ya H5N1 – aina ya homa ya ndege, huku upimaji zaidi wa kina wa chembe za urithi za virusi hivyo ukiendelea
Idadi kamili ya paka ambao wameambukizwa au kufa kutokana na ugonjwa huo bado haijulikani kwani sio visa vyote vinavyoaminika kuripotiwa.
Mnamo Juni 19,kliniki ya SpecVet magharibi mwa Poland ilitoa taarifa kwamba kulikuwa na ripoti zaidi ya 70 za ugonjwa huo nchini kote.
Ongezeko kama hilo la vifo vya paka lilitokea nchini Uingereza mnamo 2021, wakati zaidi ya paka 350 walikufa kutokana na ugonjwa wa kushangaza ambao wachunguzi waligundua baadaye kuwa ulitokana na chakula cha viumbe hao.




Discussion about this post