NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amefanya kikao na Shirika la Sayansi na Teknolojia la Anga la China (CASC) ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Serikali katika kujenga na kukuza uchumi wa kidijitali.
Hata hivyo Nape aliongoza na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maafisa kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Tume ya TEHAMA Tanzania (ICTC) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Shirika la habari la China (CRI) Juni 28,2023 imeeleza kuwa CASC ni mkandarasi mkuu wa anga za juu wa China ambaye amefanya majaribio kadhaa yenye mafanikio ya kupeleka chombo cha anga za juu kama sehemu ya mipango ya kukusanya sampuli za asteroid na kuzileta salama duniani.
Hata hivyo CRI ilimnukuu Waziri Nape akisema kwa ufupi baada ya mkutano huo kuwa pande hizo mbili zinalenga kuimarisha ushirikiano katika teknolojia ya anga ya juu na ulinzi wa taarifa binafsi.
“Hii ni sehemu ya mikakati ya serikali katika kujenga na kukuza uchumi wa kidijitali ambao utatoa maisha bora kwa Watanzania kupitia TEHAMA,” amesema Nape
Hatua hiyo mpya imekuja kufuatia uamuzi wa China wa kupanua sera yake ya diplomasia ya anga ya juu kwa kuzikaribisha nchi mbalimbali hasa nchi za Afrika kuchangamkia fursa zinazopatikana katika uchunguzi wa anga, kuboresha sayansi na kuzalisha wanaanga wengi.




Discussion about this post