NA MWANDISHI WETU,DODOMA
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Jeshi la Kujenga Taifa kuhakikisha wanafanya uwekezaji zaidi katika kufundisha vijana matumizi ya teknolojia katika shughuli zake mbalimbali za uzalishaji mali na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Makamu wa Rais amesema hayo Julai Mosi,2023 wakati wa Ufunguzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Kujenga Taifa na Maonesho ya JKT yanayofanyika katika Viwanja vya Suma JKT House eneo la Medeli Mashariki Jijini Dodoma.
Amesema ulimwengu wa sasa ni wakutumia teknolojia na akili zaidi kwa kuwa matumizi ya teknolojia yamedhihirisha uwezo mkubwa wa kuwezesha na kurahisisha utendaji kazi katika nyanja mbalimbali.
Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito kwa JKT kuona umuhimu wa kuwatambua wataalam wake wabunifuni na kuwapa tuzo sambamba na kushirikiana na Taasisi husika kuwa na haki miliki ya ubunifu na gunduzi mbalimbali zinazofanywa na Jeshi hilo.
Aidha amesema katika kutekeleza dhima ya kuwaandaa vijana wa Tanzania ili kuwajengea nidhamu, uzalendo, ukakamavu na kuwafundisha ujuzi na hatimaye kuchangia katika ulinzi wa Taifa na maendeleo ya kiuchumi, hapana budi kuweka mkazo katika suala la ulinzi na uhifadhi wa mazingira.
Ameongeza kuwa juhudi za kupanda miti na uhifadhi wa mazingira zifanywe na Kambi zote za JKT nchini, ili kuhakisha mazingira yanatunzwa kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesisitiza juu ya matumizi ya nishati safi ili kupunguza ukataji miti ovyo pamoja na kutoa msisitizo kwa JKT kuunga mkono udhibiti wa taka za plastiki, kwani huchangia kwa kiasi kikubwa katika uchafuzi wa mazingira.
Hata hivyo amelitaka Jeshi hilo kuhakikisha wanashirikiana na Taasisi zingine katika kutafuta suluhisho la upatikanaji wa chakula cha samaki hapa nchini na kusisitiza taasisi za kifedha ikiwemo mabenki kutoa elimu kwa Vijana wa JKT na kuwawezesha upatikanaji wa mikopo ili waweze kujiajiri pindi wanapohitimu mafunzo yao.
Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa amesema Wizara itaendelea kuijengea JKT uwezo ili kuweza kuongeza uzalishaji wake kupitia Suma JKT na kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati.
Amesema kwa kushirikiana na Wizara zingine za kisekta wanatarajia kuboresha mafunzo ya stadi za kazi kwa vijana wa JKT na kuwawezesha kuwapatia ujuzi na maarifa zaidi ili baada ya kuhitimu waweze kujitegemea kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za ujasiriamali.
Waziri Bashungwa ameongeza kwamba pamoja na malezi kwa vijana JKT inapaswa kuwa na ubunifu na kutoa mchango kwa taifa, kuzalisha ajira na kulisaidia taifa kuwa na chakula toshelevu.
Awali akitoa taarifa juu ya Maendeleo ya Jeshi la Kujenga Taifa, Mkuu wa Jeshi hilo Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema licha ya changamoto mbalimbali JKT imefanikiwa kufikia dhumuni la kuanzishwa kwake kwa kutoa mafunzo ya malezi kwa vijana ili kuwajengea uzalendo, kujitegemea na kuleta maendeleo endelevu na utangamano wa kitaifa.
Ameeleza kuwa malengo hayo yametekelezwa kwa ufanisi na kufanikiwa kuwabadili vijana kifikra, kuwajenga katika hali ya umoja, moyo wa kupenda kazi, uadilifu, nidhamu, uzalendo na uelewano bila kubaguana kwa misingi ya ukabila, udini, jinsia na kudumisha uhuru na amani ya Taifa.
Meja Jenerali Mabele ameishukuru serikali kwa kuendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto za Jeshi hilo ikiwemo kuendelea kutenga fedha ili kuboresha miundombinu itakayowezesha kuchukua vijana wengi zaidi kwaajili ya mafunzo.




Discussion about this post