NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya Tanzania imesema inaunga mkono jitihada za kikanda za kuimarisha hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwemo Kaskazini mwa Jamhuri ya Msumbiji
Hata hivyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kuchangia hali na mali katika misheni ya SAMIDRC ili kuhakikisha kanda inatimiza malengo yake
Hayo yameelezwa na Makamu wa Rais wa Dkt. Philip Mpango Julai 11,2023 wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Organ Troika), Utatu wa SADC (SADC Troika) na nchi za SADC zinazochangia vikosi vya kijeshi katika nchi za Jamhuri ya Kidemkorasia ya Kongo na Jamhuri ya Msumbiji.
Mkutano huo ambao umefanyika kwa njia ya mtandao umelenga kuangazia hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Kaskazini mwa Jamhuri ya Msumbiji.
Akizungumza katika Mkutano huo,Makamu wa Rais Dkt.Mpango amesema Tanzania inaunga mkono jitihada za kanda za kuimarisha hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Amesema analipongeza taifa hilo kwa utayari wake wa kutoa mchango wa ziada katika uanzishwaji wa Misheni ya SADC nchini humo (SAMIDRC).
“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kuchangia hali na mali katika misheni ya SAMIDRC ili kuhakikisha kanda inatimiza malengo yake”amesema Dkt.Mpango
Katika hatua nyingine mkutano huo umeridhia kuongezwa kwa muda wa vikosi vya misheni ya SADC nchini Musumbiji (SAMIM) kwa miezi 12 kutoka Julai 16 2023.
Mkutano huo umehudhuriwa na marais nane kutoka nchi za Kusini mwa Afrika wakiwemo Rais wa Namibia Dkt. Hage Geingob, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, Rais wa Malawi Dkt. Lazarus Chakwera, Rais wa Msumbiji Felipe Nyusi, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema,
Marais wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi, Rais wa Zimbabwe Dkt. Emmerson Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi, Waziri Mkuu wa Lesotho Samuel Ntsokoane pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Angola Balozi Te’te Antònio.




Discussion about this post