NA MWANDISHI WETU
SERIKALI kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeandaa Mwongozo wa Uingizaji, Matumizi na Utupaji Salama wa Zebaki.
Hayo yamezungunzwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis Agosti 22,2023 jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hatua zilizofikiwa juu ya uratibu na utekelezaji wa Mpango-kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki (2020 – 2025) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira.
Amebainisha kuwa Mwongozo huo unalenga kutoa utaratibu wa njia salama za usimamizi wa Zebaki pasipo kuathiri afya ya binadamu na mazingira.
Hata hivyo amesema utafiti walioufanya kuhusu teknolojia mbadala wa zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini umeonesha kuwa teknolojia za kuchoma (smelting) kwa kutumia borax na teknolojia za sianadi (cyanidation) ndio zinatumika kwa wingi nchini na nchi zinazoendelea.
Khamis ameongeza kuwa Mradi wa Kudhibiti Athari za Zebaki kwa Afya ya Binadamu na Mazingira Kwenye Shughuli za Uchimbaji Mdogo wa Dhahabu Nchini umejikita katika kufanyia kazi teknolojia zinazotumika zaidi nchini.
”Lengo ni kutekeleza malengo la Mkataba wa Minamata hususan kipengele cha saba kinachohusu kupunguza matumizi ya zebaki kwenye uzalishaji wa dhahabu inayozalishwa na wachimbaji wadogo na pale itakapowezekana kuondoa kabisa matumizi ya kemikali hiyo katika kuzalisha dhahabu kwa wachimbaji wadogo,” amefafanua Khamis
Hata hivyo ametaja shughuli za mradi huo kuwa ni kuimarisha na kujenga uwezo na ujuzi wa taasisi na wachimbaji wadogo kuhusu namna ya kudhibiti athari zinazotokana na utumiaji wa zebaki kwenye uzalishaji wa dhahabu.
Mradi huo wa miaka minne unafadhiliwa na Global Environmetal Facility (GEF) kwa ruzuku ya Sh.Bilioni 18.3 ambapo unatekelezwa katika mikoa saba ya Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga, Singida, Mbeya na Songwe.




Discussion about this post