NA MWANDISHI WETU
NAIBU Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi Mh.Crecensia Kisongo ameamuru mwadishi wa habari wa Bajeti Communication Goodluck Hongo kupelekwa mbele ya Ofisi ya Afisa Utumishi wa Mahakama hiyo ili iweze kuhakiki kitambulisho chake (press card) baada ya kutaka kuripoti kesi ya Rufaa namba 253/2022 inayomhusu Lydia Paulo Lugaga dhidi ya Damas Daniel Ndumbaro.
Uamuzi huo umetolewa Septemba 11,2023 jijini Dar es Salaam wakati rufaa hiyo ilipoanza kusikilizwa muda mfupi baada ya Karani wa Mahakama kuwaita wahusika wa shauri hilo kwa kutumia kipaza sauti kama ilivyo utaratibu wa kila siku wa kuitwa kwa mashauri mbalimbali katika mahakama hiyo.
Mara baada ya kuingia katika chumba cha mahakama ,Wakili anayemtetea Damas Ndumbaro, Neema Masawe aliieleza Mahakama hiyo kuwa kuna mtu aliyeingia ndani ya Mahakama hiyo ajitambulisha yeye ni nani ili ahafamike kabla ya kesi kuendelea.
Hata hivyo Hongo alijitambulisha mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo Mhe.Kisongo kuwa yeye ni mwanahabari na yupo hapo kusikiliza na kuripoti shauri hilo,
Lakini Masawe aliiambia Mahakama hiyo kuwa kesi hiyo inamhusu Mheshimiwa Waziri hivyo haitakiwi kuripotiwa na vyombo vya habari.
“Mheshimiwa kesi hii inamhusu mheshimiwa Waziri hivyo haitakiwi kuripotiwa na vyombo vya habari,lakini hata hivyo ipo Chamber court”amesema Masawe
Mara baada ya kauli hiyo,Naibu Msajili Mfawidhi Kisongo alipitia kitambulisho cha mwandishi huyo na kisha kumwelekeza Karani wa Mahakama kuongozana naye hadi kwa Afisa Utumishi ili aweze kukihakiki.
“Peleka kwa Afisa Utumishi aweze kuhakiki hiki kitambulisho nawe mfuate huko”amesema Naibu Msajili Mfawidhi Kisongo
Hata hivyo Ofisi ya Afisa Utumishi ilikuwa imefungwa na badala yake Karani huyo alielekea katika Ofisi nyingine ya Afisa Utumishi ambayo ilikuwa na watu na baada ya kuonesha press card hiyo alishauriwa kumwambia mwandishi huyo kuwa atoke nje na kisha kuwasubiri mawakili wa pande zote ndipo awahoji.
“Umeambiwa utoke nje kule chini na uwasubiri mawakili wote wakishatoka ndio uwahoji, nimeambiwa hivyo nikwambie”amesema Karani wa Mahakama hiyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana.
Akizungumza mara baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, Wakili upande wa mlalamikaji Pasensa Dickson amesema wapo hapo baada ya kupeleka Shauri la Rufaa la Mgogoro wa Ardhi ambalo lilifunguliwa katika Baraza la Ardhi la Wilaya ya Ilala,
Amesema katika shauri hilo Lydia Lugaga alilalamika kuwa eneo lake lilivamiwa na Damas Daniel Ndumbaro ambapo alipeleka ushahidi wake wa jinsi alivyonunua eneo hilo na waliohusika kumsaidia kulipata kwa vielelezo lakini pia Damas Ndumbaro naye alipeleka ushahidi wake na ndiye aliyekuwa shahidi pekee kwa upande wake.
“Baada ya hapo Baraza lilitoa uamuzi wake ambao ulitupilia mbali madai ya Lydia lakini baada ya kufuatilia nakala ya hukumu na kuipitia upya niligundua kuwa kulikuwa na dosari kama nane yaliyonifanya tukate rufaa”
“Baada ya rufaa tulipangiwa Naibu Msajili Mfawidhi Kisongo ili ianze kusikilizwa lakini ilichelewa kutokana na wakili upande wa utetezi kutokufika mahakamani kutokana na sababu mbalimbali ambazo Mahakama iliambiwa”amesema Dickson
Dickson ameongeza kuwa kwa sasa Mahakama imeamua kesi hiyo isikilizwe kwa njia ya maandishi badala ya ile ya kawaida ambapo taratibu hizo zitaendelea tena mwezi Oktoba,2023
“Awali sisi tulipinga kesi hiyo kusikilizwa kwa maandishi lakini sasa imeamriwa tutaisikiliza kesi hiyo kwa njia ya maandishi,basi sisi tutafanya hivyo kama sheria inavyotaka na kisha Mahakama itapitia na itatoa uamuzi wake”amesema Dickson
Akizungumzia tukio la mwandishi, kufikishwa kwa Ofisa Utumishi,Afisa Uhusiano wa Mahakama hiyo Vicent Tiganya amesema wao wanafuatilia kujua hali ilivyokuwa na kwamba watamjulisha mwandishi juu ya hatua waliyofikia
“Nipo safarini Morogoro lakini nimelipokea na nitakupigia simu,nitakujulisha”amesema Tiganya




Discussion about this post