NA MWANDISHI WETU,DODOMA
MENEJA Usimamizi wa Miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia kutoka Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Dkt. Daniel Pouakouyou amesema UNEP itaendelea kuwa mshirika wa Tanzania katika ufadhili wa miradi ya mazingira.
Kauli hiyo ameitoa katika Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma Novemba 22, 2023 wakati alipofanya mazungumzo na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga
Mbali na hilo lakini pia viongozi hao wamejadili utekelezaji wa Mradi wa Urejeshaji wa Uoto wa Asili na Uhifadhi wa Bioanuai (SLR) na kufanya mapitio ya vipaumbele vya miradi mipya ya mazingira inayoandaliwa na Tanzania kwa kushirikiana na UNEP.
Dkt. Pouakouyou amesema UNEP itaendelea kuwa mshirika wa Tanzania katika ufadhili wa miradi ya mazingira ukiwemo mradi wa SLR unaotekelezwa katika Mikoa 5 nchini iliyopo katika Mabonde ya Mto Ruaha na Bonde la Ziwa Rukwa ikijumuisha wilaya za Iringa, Wanging’ombe, Mbarali, Mbeya, Sumbawanga, Tanganyika na Mpibwe.
Ameongeza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuangalia vipaumbele vya miradi mipya ya mazingira inayofadhiliwa na UNEP na kuona maeneo mahsusi yanayohitaji ushirikiano wa karibu baina ya shirika hilo na Serikali ikiwemo upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo.
“Tunashukuru ushirikiano tunaendelea kuupata kutoka kwa Serikali. UNEP itaendelea kufadhili miradi mipya ya mazingira ikiwemo mradi wa uhifadhi wa maeneo ya ardhi oevu katika mfumo ikolojia ya bonde la Mto Wami-Ruvu ambalo ni moja ya vyanzo vikuu cha maji kwa Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na maeneo ya jirani” amesema Dkt. Poukouyou.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga amemueleza Dkt. Poukouyou dhamira na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko wa mazingira ikiwemo urejeshaji wa uoto wa asili katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Tunaishukuru UNEP kwa kuendelea kufadhili miradi ya mazingira hapa nchini, tumeandaa Mpango Kabambe wa Mazingira wa mwaka 2022-2032 ambapo moja ya maeneo ya kipaumbele ni pamoja na urejeshaji wa uoto wa asili, bioanuai na kuboresha hali ya mifumo-ikolojia na kujenga uwezo wa jamii kuwa na shughuli endelevu za uzalishaji” amesema Maganga.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Wataalamu mbalimbali kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Ofisi akiwemo Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Dkt. Paul Deogratius,Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa SLR, Dkt. Damas Mapunda na Afisa Mazingira Mwandamizi, Thomas Chali.




Discussion about this post