NA MWANDISHI WETU
MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Ardhi inatarajiwa kutoa hukumu kesi ya Rufaa namba 253/2022 inayomhusu Lydia Paulo Lugaga dhidi ya Damas Daniel Ndumbaro Desemba 5,2023 baada ya kuahirishwa mara tatu.
Kesi hiyo ya mgogoro wa ardhi iliyo chini ya Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Division ya Ardhi Crecensia Kisongo ilitarajiwa kutolewa hukumu mnamo Novemba 23,2023 baada ya kusikilizwa kwa njia ya maandishi kwa pande zote kukamilisha taratibu zilizohitajika.
Uamuzi wa kusikilizwa shauri hilo kwa njia ya maandishi ulifikiwa Septemba 11,2023 baada ya wakili wa Damas Ndumbaro,Neema Masawe kuiomba Mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo kwa njia ya maandishi.
Wakili upande wa mlalamikaji Pasensa Dickson amesema Oktoba 17,2023 waliitwa ili kuendelea na shauri hilo ambapo upande unaolalamikiwa ulishakamilisha utaratibu wote kama unavyohitajika katika kesi zinazosikilizwa kwa njia ya maandishi baada ya wao nao kukamilisha.
“Sasa baada ya hapo ilitakiwa kutolewa hukumu Novemba 23,2023 lakini iliahirishwa na kupelekwa Novemba 28,2023 lakini pia iliahirishwa hadi nilipopigiwa simu na karani Desemba 4,2023 kuwa hukumu itatolewa saa tano”amesema Dickson.
Hata hivyo hukumu hiyo iliahirishwa tena na itatolewa Desemba 5,2023 hivyo kuifannya hukumu hiyo kuahirishwa mara tatu.
Pande zote zimeshakamilisha taratibu za kimahakama hivyo wanasubiri uamuzi baada ya mahakama kujiridhisha kwa ushahidi wa pande zote mbili.
Septemba 11,2023,Mahakama hiyo iliamuru mwadishi wa habari wa Bajeti Communication Goodluck Hongo kupelekwa mbele ya Ofisi ya Afisa Utumishi wa Mahakama hiyo ili iweze kuhakiki kitambulisho chake (press card) baada ya kutaka kuripoti kesi ya Rufaa namba 253/2022 inayomhusu Lydia Paulo Lugaga dhidi ya Damas Daniel Ndumbaro.
Uamuzi huo ulikuja wakati rufaa hiyo ilipoanza kusikilizwa muda mfupi baada ya Karani wa Mahakama kuwaita wahusika wa shauri hilo kwa kutumia kipaza sauti kama ilivyo utaratibu wa kila siku wa kuitwa kwa mashauri mbalimbali katika mahakama hiyo.
Mara baada ya kuingia katika chumba cha mahakama ,Wakili anayemtetea Damas Ndumbaro, Neema Massame aliieleza Mahakama hiyo kuwa kuna mtu aliyeingia ndani ya Mahakama hiyo ajitambulishe yeye ni nani ili afahamike kabla ya kesi kuendelea.
Hata hivyo Hongo alijitambulisha mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo Kisongo kuwa yeye ni mwanahabari na yupo hapo kusikiliza na kuripoti shauri hilo,
Lakini Massame aliiambia Mahakama hiyo kuwa kesi hiyo inamhusu Mheshimiwa Waziri hivyo haitakiwi kuripotiwa na vyombo vya habari.
“Mheshimiwa kesi hii inamhusu mheshimiwa Waziri hivyo haitakiwi kuripotiwa na vyombo vya habari,lakini hata hivyo ipo “Chamber court”amesema Massame
Mara baada ya kauli hiyo,Naibu Msajili Mfawidhi Kisongo alipitia kitambulisho cha mwandishi huyo na kisha kumwelekeza Karani wa Mahakama kuongozana naye hadi kwa Afisa Utumishi ili aweze kukihakiki.
“Peleka kwa Afisa Utumishi aweze kuhakiki hiki kitambulisho nawe mfuate huko”amesema Naibu Msajili Mfawidhi Kisongo
Hata hivyo Ofisi ya Afisa Utumishi ilikuwa imefungwa na badala yake Karani huyo alielekea katika Ofisi nyingine ya Afisa Utumishi ambayo ilikuwa na watu na baada ya kuonesha press card hiyo alishauriwa kumwambia mwandishi huyo kuwa atoke nje na kisha kuwasubiri mawakili wa pande zote ndipo awahoji.
“Umeambiwa utoke nje kule chini na uwasubiri mawakili wote wakishatoka ndio uwahoji, nimeambiwa hivyo nikwambie”amesema Karani wa Mahakama hiyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana.




Discussion about this post