NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar,kimesema wananchi wanahitaji siasa za kuvumiliana na ustaarabu ikiwemo wanavyonufaika kiuchumi na kijamii huku nchi ikipiga hatua kubwa za maendeleo.
Hata hivyo wanachama na viongozi wa chama hicho wametakiwa kujibu hoja kwa hoja huku wakitangaza na kuhamasisha kwa kasi kubwa mambo yaliyotekelezwa na Serikali mijini na vijijini kwa maslahi ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Machi 11,2024 na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,wakati akizungumza na wanachama na viongozi wa Chama hicho huko Jimbo la Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja Visiwani Zanzibar.
Dkt.Dimwa amesema vyama vya siasa Zanzibar vimepoteza muelekeo na mvuto kwa wananchi kutokana na kasi kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya mwaka 2020-2025.
Ameongeza kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wanatumia vibaya uhuru wa kutoa maoni na badala yake wanatoa kauli za kumdhalilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ally Mwinyi huku wakipandikiza kauli za uchochezi kwa wananchi.
Hata hivyo Dkt.Dimwa,amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria wanasiasa hao na watu wengine wanaovunja sheria kwa makusudi kwa kumdhalilisha Rais wa Zanzibar ikiwemo kuthibiti upotoshaji unaondikwa katika mitandao ya kijamii nchini kwa lengo la kumdhalilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Aidha amebainisha kuwa CCM itaendelea kulinda kwa vitendo heshima,hadhi thamani ya Rais wa Zanzibar na wasaidizi wake kwani wapo katika mamlaka yanayotokana na Chama Tawala cha CCM kupitia ridhaa halali ya uchaguzi wa Kidemokrasia chini ya matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
“Juzi Chama Cha ACT-Wazalendo wamefanya mapokezi ya Viongozi wao lakini jambo la kusikitisha mikutano yao kwa Unguja na Pemba imepambwa na kauli chafu dhidi ya Rais wetu mpendwa Dk.Hussein Mwinyi,hatuwezi kuvumilia utovu huo wa nidhamu kwani haukubaliki kisiasa,kidini na kitamaduni.
”Tabia hizo zinafanya tuanze kutilia mashaka kama kweli wenzetu wana nia ya dhati ya kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) au wana ajenda zao binafsi kuirejesha Zanzibar katika machafuko ya kisiasa”,amesema Dkt.Dimwa.




Discussion about this post