NA MWANDISHI WETU ZANZIBAR
UWANJA wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume wa visiwani Zanzibar umetangazwa kuwa moja ya viwanja bora zaidi vya ndege barani Afrika.
Hayo yameelezezwa Machi 15,2024 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, Seif Abdallah Juma baada ya uwanja huo kutunukiwa tuzo za Ubora wa Huduma za Viwanja vya Ndege zinazotolewa na Baraza la Viwanja vya Ndege Kimataifa ambayo ni taasisi inayojihusisha na huduma za viwanja vya ndege kwa lengo la kuunganisha utendaji wa sekta hiyo kwa viwango vya kimataifa
Amesema tuzo hizo za Ubora wa Huduma za Viwanja vya Ndege zinazotolewa na Baraza la Viwanja vya Ndege Kimataifa hutolewa kila mwaka na zinazingatia ubora wa uwanja wa ndege kulingana na maoni ya abiria yaliyokusanywa kupitia tafiti za kila siku katika maeneo ya kuondoka na kuwasili abiria hao kote duniani
”Tuzo hizo zinazingatia ubora wa uwanja wa ndege kulingana na maoni ya abiria yaliyokusanywa kupitia tafiti za kila siku katika maeneo ya kuondoka na kuwasili abiria hao kote ulimwenguni na hii itaongeza idadi ya watalii wanaotembelea visiwa vya Zanzibar”amesema Juma
Aidha ameongeza kuwa tuzo hizo zinatolewa kwa kuzingatia vielelezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na wafanyakazi waliojitolea zaidi, wepesi zaidi wa safari kwenye uwanja wa ndege, uwanja wa ndege wenye mvuto zaidi na uwanja wa ndege msafi zaidi.
” Mafanikio haya yametokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika kuvutia uwekezaji mkubwa kwenye sekta hiyo”amesema Juma
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ndio uwanja wa ndege pekee wa kimataifa visiwani Zanzibar ambapo watalii wengi huwasili visiwani Zanzibar humo kila mwaka kutokana na vivutio vyake vya kila aina yakiwemo maeneo ya kale na fukwe za kuvutia




Discussion about this post