NA GOODLUCK HONGO
SERIKALI ya Tanzania imo katika hatua ya mwisho ya kuwashirikisha wananchi matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ili waweze kupanga mipango yao ya kimaendeleo ikiwemo kiuchumi kijamii na kisiasa katika maeneo yao kuanzia ngazi ya Kata,Kijiji na Kitongoji
Hayo yameelezwa mkoani Dar es Salaam na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Anne Makinda wakati wa Mafunzo kwa Wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaa (DCPC) kuhusu Usambazaji na Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 yaliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) yaliyofanyika Machi 13 na 14,2024.
Amesema Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni tofauti na Sensa za miaka iliyopita ambapo baada ya kufanyika hakuna tena muendelezo wake kwa wananchi lakini safari hii Rais Samia Suluhu Hassan alizindua Mwongozo wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ambapo sasa matokeo hayo yanawafikia wananchi kuanzia ngazi za chini kwa uwazi.
Amesema hiyo ni Sensa ya sita kufanyika nchini ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni kutangazwa na kuhamasisha na awamu ya pili ni kufanyika kwa Sensa hiyo ambapo sasa ni awamu ya tatu kwa wananchi kupata matokeo hayo ili kupanga mipango ya maendeleo na serikali katika maeneo yao.
‘’Kila mwananchi anauwezo wa kujua taarifa katika Kijiji chake na wanasiasa shangilie lakini Sensa ni kiboko kwa kuwa kwenye takwimu hakuna makandokando kwani Sensa hii inaonesha kila kitu kuanzia ngazi ya chini hivyo wananchi wanapojua matokeo ya Sensa katika eneo lao itasadia kuzungumza wanachodai’’amesema Makinda
Aidha amebainisha kuwa sekta ya habari ni daraja muhimu kati ya wananchi na Serikali na ina mchango wa kipekee katika kuleta maendeleo ya kiuchumi,kisiasa,kijamii ambapo ilifanya kazi kubwa wakati wa kuanza kwa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
‘’Mafanikio ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni mfano bora wa kazi iliyofanywa na vyombo vya habari na sisi tunawafundisha Wakuu wa Mikoa,Madiwani,Makatibu Wakuu,Wakuu wa Wilaya juu ya matokeo hayo kwani humo kuna matokeo mengi sana hivyo hata waandishi wa habari itawasaidia zaidi katika kufanya kazi zenu’’ameongeza Makinda
Akizungumza kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt.Albina Chuwa,Meneja wa Takwimu na Mratibu wa Sensa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Kapala amesema waandishi wa habari ni watu muhimu katika zoezi hilo kwa kuwa wanasaidia kufikisha taarifa za sensa kwa watu wa hali ya chini
Naye Mwenyekiti wa DCPC Samson Kamalamo ameishukuru Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari Mkoa wa Dar es Salaam ili kuwa sehemu ya mapango wa utekelezaji wa awamu ya tatu ya kuwafikisha wananchi matokeo hayo ya Sensa ya Mwaka 2022.
‘’Naishukuru sana Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kuishirikisha DCPC kwa kuwa inagusa asilimia 75 ya vyombo vyote vya habari Tanzania na tunafurahi kuona vyombo vya habari ni muhimu katika utekelezaji wa awamu hii ya tatu ya usambazaji na matumizi ya matokeo hayo wananchi’’amesema Kamalamo




Discussion about this post