NEW DELH,INDIA
JIJI la Mumbai nchini India limetajwa kuwa ndio jiji linalokaliwa na mabilionea wengi katika Bara la Asia na kushika nafasi ya tatu duniani baada ya New York la Marekani na London nchini Uingereza.
Mumbai umeipiku Jiji la Beijing nchini China na kuwa ‘mji mkuu wa mabilionea’ wa Asia kwa mara ya kwanza.
Kulingana na Taasisi ya Utafiti ya Hurun yenye makao yake makuu Shanghai nchini China,imeeleza kuwa idadi ya mabilionea katika kitovu cha kifedha cha India ilipanda hadi 92, na kushika namba tatu juu zaidi ulimwenguni baada ya New York inayokaliwa na mabilionea 119 na London 97.
Hata hivyo, Mji Mkuu wa India New Delhi umeingia kwenye 10 bora kwa mara ya kwanza.
Kulingana na taasisi hiyo India ina mabilionea 271, ambayo ni ya tatu kwa juu zaidi duniani, nyuma ya China 814 na Marekani 800.
Mmiliki wa Kampuni ya India Reliance Industries Mukesh Ambani , amebaki na nafasi yake kama Mhindi tajiri zaidi na ana utajiri wa dola za kimarekani Bilioni 115, ambayo pia inamfanya kuwa mtu tajiri zaidi barani Asia.
Tajiri wa pili kwenye orodha hiyo ni Mwenyekiti wa Adani Gautam Adani mwenye utajiri wa (dola za kimarekani bilioni 86), ambaye utajiri wake umeongezeka kwa asilimia 33.
Mwenyekiti na Mtafiti Mkuu wa Ripoti ya Hurun Rupert Hoogewerf amesema akili ya bandia (AI) imekuwa kichocheo kikuu cha mwenendo huo, ikizalisha zaidi ya nusu ya utajiri wote mpya mwaka huu.
Idadi ya mabilionea nchini India imeongezeka kwa kasi tangu nchi hiyo ilipofanyia mageuzi sera yake ya kiuchumi mwaka 1991 ili kuruhusu uwekezaji zaidi wa kigeni.
Hata hivyo, tofauti ya utajiri kati ya asilimiamoja ya juu na maeneo mengine ya nchi imefikia viwango vya juu vya kihistoria.



Discussion about this post