NA MWANDISHI WETU
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika mara baada ya athari za ugonjwa wa Uviko19 ambapo umekua kwa asilimia 5.5 kwa mwaka 2023 na kutarajiwa kukuka kwa asilimia 6 kwa mwaka 2024-2027.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika kujenga uchumi imara kupitia R nne zinazolenga Uhimilivu, Ujenzi Mpya, Maridhiano na Mageuzi.
Halikadhalika Dkt.Mpango amesema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ili kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara na uwekezaji.
Dkt.Mpango ameseyama hayo Machi 27,2024 wakati akifunga Jukwaa la Uwekezaji kati ya China na Tanzania lililofanyika Jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa Tanzania imedumisha amani tangu kupata uhuru mwaka 1961, na imeendelea kufanya mageuzi ya sheria na utekelezaji sera zinazolenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara.
Ametaja uwekezaji huo ni pamoja na miradi ya nishati ya uhakika, uboreshaji bandari, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambayo itafika hadi Burundi na Kindu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwemo na elimu ili kupata rasilimali watu iliyobora zaidi pamoja na sekta ya afya.
”Tunawakaribisha wawekezaji kutoka nchini China na mataifa mengine kuwekeza nchini Tanzania kutokana na mazingira rafiki ya kijiografia, kimiundombinu, kisiasa, kisera na kisheria yaliyopo.
”Tunawasihi wawekezaji kutoka China na Mataifa mengine kuwekeza Tanzania katika mazingira na uchumi wa buluu,na kuendeleza maeneo ya pwani na visiwa ili kuweza kutumia vema uchumi wa buluu na huku mazingira yakilindwa kwa kuja na teknolojia za kisasa zitakazosaidia kuwahamisha wananchi katika matumizi ya nishati chafu na kuokoa uharibifu wa mazingira.
”Faida za kijiogragfia ni pamoja na kuwa na soko la ndani la watu zaidi ya milioni 64 pamoja na soko la watu Bilioni 1.4 katika matumizi ya Ukanda Huru wa Biashara Barani Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki”amesema Dkt.Mpango
Aidha ameongeza kuwa, Uwekezaji nchini Tanzania unawezesha kufikia masoko ya Marekani kupitia mpango wa AGOA, soko la Ulaya kupitia mpango wa EBA pamoja na soko la China kupitia mpango wa FOCAC, pia nchi za Japan kupitia TICAD pamoja na soko la India.

Hata hivyo Makamu wa Rais Dkt Mpango amesema kwa muda mrefu Jamhuri ya Watu wa China imekuwa mwekezaji mkuu wa kimkakati na mshirika wa biashara wa Tanzania. Na kubainisha kuwa mtiririko wa fedha wa kila mwaka kutoka China uliongezeka kutoka Dola za Kimarekani Milioni 92 mwaka 2019 hadi dola Milioni 221 mwaka 2021.
”Katika kipindi cha Januari 2021 hadi Desemba 2023, miradi 256 ya Kichina iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania ikiwa na thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 2.4, huku ikikadiriwa kuzalisha ajira 29,122”amesema Dkt.Mpango




Discussion about this post