MWANDISHI WETU,IRINGA.
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA),imewataka waandishi wa habari nchini kuendelea kuandika habari za dawa, vifaa tiba na bidhaa za tumbaku zenye kuleta tija kwa jamii.
Aidha TMDA inatambua kazi kubwa inayofanywa na waandishi wa habari katika kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Dawa na vifaa tiba ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza endapo dawa hizo hazitatumiwa ipasavyo.
Wito huo umetolewa Mei 17,2024 mkoani Iringa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA Dkt. Adam Fimbo wakati wa utoaji wa tuzo kwa waandishi wa habari bora wa Uandishi wa Habari za Dawa, Vifaa Tiba, Vitendanishi na Bidhaa za Tumbaku kwa mwaka 2024 .
Amesema TMDA inatambua mchango wa waandishi wa habari hivyo kuifanya Mamlaka hiyo kuandaa tuzo kwa wanahabari watanaondika habari za TMDA zenye kuleta tija kwa jamii
Ameongeza kuwa tuzo hizo ni sehemu ya jitihada za TMDA wanazozifanya kwa waandishi wa habari katika kuripoti habari za dawa, vifaa tiba, bidhaa za tumbaku na vitendanishi katika kuuhabarisha umma wa watanzania.
“Tunataka mtuandike mambo yote ambayo mmeyachunguza vizuri yaandikwe ili tujirekebishe.
“Tuzo hizi ni maazimio ya kikao kazi yaliyofanyika mkoani Arusha Mwaka 2021 ambapo Mwaka 2022 tulianza utekelezaji wake,”amesema Dkt.Fimbo
Hata hivyo Dkt.Fimbo amewahimiza waandishi wa habari kuendelea kuelimisha jamii bila kuchoka kwani wana nafasi kubwa ya kuwafikia Wananchi.

Waandishi walioshinda tuzo hizo ni Veronica Mrema kutoka blogu ya Matukio na Maisha, ,Madina Mohammed wa blogu ya Wamachinga TV, Penina Malundo kutoka Times Majira na mshindi wa nne akiwa ni Andrew Chale wa Matukio Daima
Utoaji wa tuzo hizo pia uliambatana na kikao kazi cha wahariri na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura 219.




Discussion about this post