NA MWANDISHI WETU,MAGU
MKUU wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza Joshua Nassari amewataka vijana wilayani humo kuongeza juhudi katika masomo ili waweze kufikia malengo yao na kuinua kiwango cha taaluma katika eneo hilo.
Nassari ametoa kauli hiyo wilayani humo wakati akipokea vikombe vya ushindi baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu kushika nafasi ya kwanza kimkoa katika Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA).
Magu ambayo imefanya vizuri katika mshaindano hayo kwa kuchukua vikombe 13 katika fani za Mpira wa Kikapu Wavulana na Wasichana, Riadha , Kwaya, Ngoma, Mpira wa miguu wavulana, Handball , Usafi na Nidhamu pamoja na Kombe la Mshindi wa Jumla katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza zilizoshiriki mashindano hayo.
Akizungumza wakati akipokea vikombe hivyo Mei 31,2024,Nassari amewapongeza vijana hao kwa kufanya vizuri katika mashindano hayo nakuwaomba kuongeza bidii na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya Kitaifa.
Amesema ni muhimu sana kwa wanafunzi hao kutumia ushindi huo katika kuongeza juhudi na bidii katika taaluma na kufanya vizuri katika masomo yao ili kufikia malengo yao na kuifanya wilaya ifanye vizuri katika taaluma.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhani ametoa pongezi kwa wote waliofanikisha ushindi na kuwataka wafanye vizuri zaidi kwa mashindano mengine mwaka 2025.
Awali akitangaza matokeo hayo,Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Magu, Peter Mujaya amesema Magu imebeba vikombe 13 katika fani ya Mpira wa Kikapu Wavulana na Wasichana nafasi ya kwanza, Mpira wa mikono wavulana nafasi ya pili, na wasichana nafasi ya tatu, Riadha wasichana nafasi ya kwanza na wavulana nafasi ya tatu.
Kwa upande wa nafasi ya Kwaya,Mujaya amebainisha kuwa wameshika nafasi ya kwanza, Ngoma nafasi ya pili , Muziki nafasi ya tatu, Mpira wa miguu nafasi ya tatu, Usafi na Nidhamu nafasi ya kwanza, Mpira wa wavu nafasi ya tatu pamoja na Kombe la Mshindi wa Jumla kwa Mkoa wa mwanza.
Vijana 26 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Magu wameteuliwa kuunda timu ya mkoa itakayoshiriki mashindano ya UMITASHUMTA Taifa yatakayofanyika mwezi Juni mkoani Tabora.




Discussion about this post