SEOUL,KOREA KUSINI
WAKATI mizozo ikiongozeka duniani kutokana na uwepo wa ushindani wa pande mbili za wale wanaoziunga mkono Marekani na washirika wake wa nchi za Magharibi na wanaoziunga mkono Urusi na washirika wake ikiwemo China,Korea Kaskazini na Kusini zimekuwa zikitumiana takataka kupitia maputo yanayorushwa angani.
Korea Kaskazini ambayo inaungwa mkono na China,Urusi na Iran inadaiwa kuwa imekuwa ikituma maputo ya takakata kuelekea Korea Kusini inayoungwa mkono na Marekani na nchi za Magharibi ambayo nayo imekuwa ikituma maelfu ya vipeperushi vinavyoipinga Serikali ya Korea Kaskazini.
Kwa mujibu wa taarifa ya tovuti ya Kituo cha habari cha Serikali ya Japan ya NHK kimeeleza kuwa Korea Kaskazini itasitisha kwa muda kutuma maputo yaliyojazwa takataka nchini Korea Kusini na kuonya kuwa inaweza kuendelea na operesheni hiyo ikiwa upande wa Korea Kusini utatuma vipeperushi zaidi vya kupinga Korea Kaskazini nchini Korea Kaskazini.
NHK imetangaza kuwa Korea Kaskazini imekuwa ikituma maputo yaliyojazwa taka tangu wiki iliyopita kwa kile kilichoelezwa kulipiza kisasi dhidi ya vitendo vya baadhi ya wanaharakati nchini Korea Kusini ambao walituma maputo yenye vipeperushi vya kukosoa uongozi wa Korea Kaskazini nchini Korea Kaskazini.
Ofisi ya Rais wa Korea Kusini ilikuwa imetoa onyo siku ya Jumapili kwamba itachukua hatua “zisizovumilika” dhidi ya Korea Kaskazini, ikiwa haitaacha kutuma maputo yaliyojazwa taka.
Muda mfupi baada ya onyo hilo la Korea Kusini,Makamu wa Waziri wa Ulinzi wa Korea Kaskazini Kim Kang Il alitangaza kwamba operesheni ya puto ilikuwa inasitishwa kwa muda na kuongeza kuwa Korea Kaskazini ilituma tani 15 za taka za karatasi.




Discussion about this post