NA ANDREW CHALE
WATOTO zaidi ya Milioni 200 wanatumikishwa katika kazi mbalimbali duniani huku Milioni 73 kati yao wakiwa chini ya umri wa miaka 10.
Hata hivyo Sekta ya Kilimo imetajwa kuongoza kwa kuajiri watoto wengi hasa katika mashamba ya chai, tumbaku, miwa, mwani, karafuu na shughuli za uvuvi.
Taarifa hiyo imetolewa wakati wa kongamano la kujadili ulinzi wa mtoto kuwa kamati lililoandaliwa na Mtandao wa Kupinga Utumikishwaji wa Watoto na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Juni 5,2024 jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo Kongamano hilo limekuja wakati Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2022 (DHS-MIS 2022) uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS) kueleza kuwa kaya za Tanzania zina wastani wa watu 4.5 huku asilimia 29 ya kaya hizo zikiongozwa na wanawake.
Utafiti huo umebainisha kuwa takribani nusu (sawa na asilimia 46) ya watu wote katika kaya hizo za Tanzania ni watoto wa umri chini ya miaka 15.
Kutokana na utafiti huo,Kongamano hilo linaweza kusaidia katika kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya utumikishwaji na vitendo vya ukatili dhidi yao yakiwemo mauaji.
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Katiba na Sheria,Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali inakwenda kuweka sheria kali zitakazomlinda mtoto hapa nchini ambapo jopo la mawaziri wa wizara zaidi ya nne watakutana kwenye Kamati Maalum.
Balozi Dkt. Chana amebainisha kuwa jopo hilo litaundwa na Kamati ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Maendeleo ya Jamii na Wizara ya Katiba na Sheria ili kuangalia chanzo ni nini kinachosababisha ukatili kwa watoto nchini.
Aidha ameongeza kuwa jopo hilo litaangalia chanzo cha ukatili huo na kisha wataweka mikakati ili kudhibiti unyanyasaji huo.
“Tumekubaliana tukutane tuweke mikakati ya kuangalia vyanzo vya ukatili kwa watoto, tutashirikiana na familia, shule, taasisi za dini ili tuweze kudhibiti ukatili.
‘’Umefika wakati wa kuweka mikakati ili kuhakikisha mtoto anapata haki zake ikiwemo ya elimu, matibabu na kulindwa dhidi ya utumikishwaji na shughuli nyingine’’amesema Balozi Dkt.Chana
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la UN Global Compact Chapa ya Tanzania, Marsha Yambi, amesema watoto Milioni 200 wanatumikishwa katika kazi mbalimbali duniani ambapo kati yao Milioni 73 wako chini ya miaka 10.
Yambi amebainisha kuwa Sekta ya Kilimo ndio inaongoza kwa kuajiri watoto wengi hasa katika mashamba ya chai, tumbaku, miwa, mwani, karafuu na shughuli za uvuvi.
“Sekta binafsi inaonekana inachangia kuajiri watoto wadogo kwenye mashamba, tuhakikishe watoto hawawi katika ajira na tupate faida kwa haki na siyo kwa kupitia watoto,” amesema Yambi.
Mratibu wa Mtandao wa Kupinga Utumikishwaji wa Watoto nchini, Scholastica Pembe, amesema kongamano hilo limelenga kujadili sera na sheria zinazomlinda mtoto na ikiwemo Sheria ya Ndoa ambayo inaruhusu mtoto aolewe chini ya miaka 18.
Pembe ameitaja Sheria ya Kazi ambayo pia inaruhusu mtoto aanze kufanya kazi kuanzia miaka 14 na kuendelea lakini afanyishwe kazi ambazo si hatarishi na apate muda wa kucheza.




Discussion about this post