NA MWANDISHI WETU
JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe kwa kipindi cha mwezi Mei, 2024 linawashikilia watuhumiwa 680 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio mbalimbali ya uvunjaji wa sheria ikiwemo mke na hawara yake kwa kuhusika na mauaji ya mume wake.
Mbali na matukio hayo lakini pia watuhumiwa hao waliokamatwa kwa nyakati tofauti,wamejihusisha pia na utapeli kwa njia ya mtandao, dawa za kulevya, ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani na kusababisha ajali za vifo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Juni 6,2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe SACP Augustino Senga amesema,Jeshi la Mkoa wa Songwe linamshikilia mke na hawara yake kwa tuhuma za mauaji ya mumewe kutokana na wivu wa kimapenzi.
Amesema watuhumiwa hao wanadaiwa kumuua Victor Mwakapenda (41) mkazi wa Mtaa wa llembo Wilaya ya Mbozi mkoani humo ambapo marehemu alitoweka nyumbani tangu Aprili 30, 2024 akiwa na mke wake wakielekea kwa mganga wa kienyeji eneo la Senjele Majimoto
Amesema baada ya safari hiyo marehemu hakuonekana tena hadi mwili wake ulipopatikana Mei 9, 2024 katika Msitu wa Mpoloto uliopo Kijiji cha Igale Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Kamanda Senga amebainisha kuwa baada ya mwili huo kutelekezwa katika msitu huo,wananchi waishio maeneo hayo waliuona na kisha taarifa zilitolewa na JeshI la Polisi kuuchukua na kuupeleka hospitali ya Ifisi jijini Mbeya na kuhifadhiwa mpaka ndugu zake walipoutambua Mei 29, 2024 na kukabidhiwa kwa ajili ya mazishi.
Aidha ameongeza kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea na pindi utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.
Wakati huo huo,Kamanda Senga ameeleza kuwa jeshi hilo linawashikilia wanaume wawili ambao ni, wakazi wa Kaloleni Wilaya ya Songwe mkoani humo wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini kwa tuhuma za kumbaka na kumuua mtoto mdogo mwenye umri wa miaka miwili na nusu mkazi wa eneo hilo
”Watuhumiwa hawa walifanya tukio hili kwa kumchukua mtoto huyo na kwenda kumbaka kwenye shamba la mahindi umbali wa mita 130 Mei 9, 2024 kutoka nyumbani kwao baada ya kuachwa na mama yake mzazi akiwa amelala alipokwenda kuchota maji kisimani.
”Uchunguzi wa awali umebaini kuwa, mauaji haya yametokana na imani za kishirikina kutokana na shughuli za watuhumiwa za uchimbaji wa madini.
”Taarifa za kupotea kwa mtoto huyo ziliripotiwa Kituo cha Polisi Mei 9, 2024 na Mei 10, 2024 kukupatikana akiwa ameuawa”amesema Kamanda Senga
Amefafanuwa kuwa upelelezi wa shauri hili bado unaendelea na pindi utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe ambao wanajihusisha na uhalifu na vitendo vya ukatili wa kijinsia kuacha mara moja kwani hawatoweza kukwepa mkono wa sheria.




Discussion about this post