NA MWANDISHI WETU,DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema kazi za Machifu katika jamii ni kusuluhisha au kuleta suluhu.
Amesema na pale inapobidi adhabu ipite basi iwe adhabu inayoendana na misingi ya haki kama ilivyo kwenye jamii.
Rais Dkt Samia ametoa kauli hiyo Ikulu Chamwino jijini Dodoma Julai 20,2024 wakati akizungumza na Machifu kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Rais Dkt.Samia ambaye pia ni Kiongozi wa Machifu nchini anayejulikana kama Chifu Hangaya amebainisha kuwa kila wanapokwenda mahali wanakutana na malalamiko mengi ya wananchi na anapotokea kiongozi wa chama au Serikali ndio wananchi wanakimbilia.
‘’Tunaomba machifu tusaidieni, nyinyi kama viongozi wa jamii mliokubalika kule,migogoro mingine hii tusaidieni.
‘’Migogoro mingi katika jamii zetu inakiuka mila na heshima za watu,jengeni mvuto kwa watu wetu waje wawakimbilie pamoja na tofauti za wanajamii lakini wote tuhakikishe tunawaongoza watu kwa maridhiano kwenye mambo tofauti tustahimiliane tufanye mabadiliko na tusonge mbele’’amesema Rais Dkt Samia (Chifu Hangaya)
Rais Dkt Samia(Chifu Hangaya) ameongeza kuwa Machifu wanadhamana ya Sheria za Kimila na wanapowaita watu na kuwahukumu kwa Sheria za Kimila watu huwa hawarudi nyuma.
‘’Sisi ndio tunaifanya jamii iheshimu misitu yetu kwani huko ndiko tunakokwenda kuomba lakini kwa yale maeneo ambayo Machifu hawafanyi kazi hii ni kukame, hakuna baraka na mvua hazinyeshi.
‘’Niliwaelekeza Wizara watengeneze muongozo ambao utawatambua Machifu na mambo yao wanayoyafanya katika maeneo yao.
‘’Kama mnamuona kiongozi haendi mwendo mwema tuambieni tumjue ili tulete viongozi waadilifu na mambo yaende vizuri”amesema Rais Dkt Samia (Chifu Hangaya)





Discussion about this post