NA MWANDISHI WETU
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amehimiza uwekezaji uliofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wa Upandikizaji Mimba pamoja na uwashaji wa vifaa vya kusaidia kusikia kwa watu wenye changamoto ya kusikia kuwa endelevu.
Makamu wa Rais Dkt.Mpango ametoa wito huo Septemba 12,2024 wakati wa hafla ya kuzindua Kituo cha Upandikizaji wa Mimba, kuwasha Vifaa vya Kusaidia Kusikia kwa Watoto na Kuzindua Gari la Huduma Tembezi za Afya (Mobile Medical Service) iliyofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Amesema ni muhimu kuondokana na utegemezi wa wataalam kutoka nje na lazima jitihada za makusudi zichukuliwe ili kuwezesha uhamishaji wa teknolojia na ubunifu.
Makamu wa Rais Dkt.Mpango ameiagiza Wizara ya Afya kuandaa mpango madhubuti wa kuwajengea uwezo wataalam wa ndani watakaoweza kuvitumia na kuvifanyia ukarabati vifaa vyote vya kisasa, pindi hitaji hilo litakapojitokeza.
‘’Uzinduzi wa huduma za upandikizaji mimba na vifaa vya usikivu ni hatua muhimu sana katika kusaidia wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya uzazi na watoto waliozaliwa wakiwa na changamoto ya usikivu.
‘’Ni faraja kuona huduma ya upandikizaji wa mimba inaanza kutolewa kwa mara ya kwanza nchini katika Hospitali ya Umma”amesema Dkt.Mpango
Aidha ameongeza kwamba hatua ya kuboresha huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kutokana na upungufu wa wataalamu bobezi au ukosefu wa vifaa vya kutolea huduma husika.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele katika kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi ambapo imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, rufaa na kanda.
‘’Sambamba na uwekezaji mkubwa unaolenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na kibobezi, Serikali imedhamiria kutekeleza kwa vitendo ajenda ya kimkakati ya kukuza utalii wa tiba hapa nchini ili kuliongezea Taifa fedha za kigeni na kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa kupitia sekta ya huduma.
”Tunampongeza na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha na kuboresha huduma za afya nchini ikiwemo upatikanaji wa vifaa tiba, wataalamu na dawa, pamoja na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya.
”Serikali imeongeza Bajeti Wizara ya Afya kutoka Sh.Bilioni 900.1 mwaka 2020/21 hadi Sh.Trilioni 1.3 mwaka 2024/25 ambapo Katika kipindi hicho, fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya afya iliongezeka kutoka asilimia 40 ya bajeti ya afya mwaka 2020/21 hadi asilimia 59 mwaka 2023/24.”amebainisha Dkt.Mpanngo
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Wizara itaendelea kushirikiana na Taasisi zinazotoa huduma za afya nchini ili malengo ya Serikali yaweze kutimia kwa ustawi wa wananchi.
Amesema Wizara itajielekeza katika kushughulikia gharama za matibabu ya kibobezi ili kuwasaidia watanzania wote kuhudumiwa.
‘’Wizara itahakikisha wakati wa matumizi ya bima ya afya kwa wote kunakuwepo na mfumo wa rufaa utakaowezesha watanzania kufikia huduma kutoka tiba msingi hadi tiba bobezi”amesema Mhagama
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika ambao utawezesha kusaidia watanzania wanaopitia changamoto za upatikanaji wa mimba pamoja na wale wenye changamoto ya kusikia.
Kuzinduliwa kwa Kituo cha Huduma ya Upandikizaji wa Mimba cha Hospitali ya Taifa Muhimbili kunaifanya hospitali hiyo kuwa ya kwanza kwa upande wa hospitali za umma kutoa huduma hiyo.




Discussion about this post