NA MWANDISHI WETU,KILIMANJARO
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kushirikiana na watafiti kutoka Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Fiziolojia na Ikolojia ya Wadudu (icipe) kutoka nchini Kenya imetoa mafunzo kwa maafisa ugani na wakulima viongozi 165 juu ya njia husishi za kudhibiti wadudu waharibifu wa matunda ya Parachichi, Machungwa na Embe.
Mafaunzo hayo yametolewa kupitia vituo vya utafiti vya Ukiriguru (Mwanza), Tengeru (Arusha) na Mlingano (Tanga) kwa maafisa ugani na wakulima viongozi 165 kutika Kata 31 za maeneo hayo
Awali akifungua mafunzo hayo Septemba 9 hadi 13, 2024 wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Wilaya hiyo Lazaro Twange ameipongeza TARI kwa kuweka nguvu ya kuwajengea uwezo wataalam wa kilimo na wakulima viongozi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuinua sekta hiyo muhimu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Muheza Dkt. Juma Mhina amebainisha kuwa mradi huo umekuja wakati sahihi na kwa watu sahihi akitolea mfano wa Muheza kuwa uchumi wa wananchi wa wilaya hiyo hutegemea machungwa na wamekuwa na kilio cha wadudu waharibifu wa matunda hayo.
Aidha Dkt. Mhina amesema mradi huo utakuwa ni suluhisho la changamoto ya wadudu waharibifu huku ikichangia kipato cha wakazi wa Muheza, kuongezeka mapato ya Halmashauri na hatimaye taifa kwa ujumla kupitia kilimo cha matunda yanayouzwa ndani na nje ya nchi.
Mtafiti Kiongozi wa Mradi huo kutoka TARI Ukiriguru Dkt, Abdullah Mkiga amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wakulima wanapata elimu bora ya kudhibiti wadudu waharibifu wa matunda kama Nzi na Nondo wanaoshambulia matunda na kusababisha matunda kuoza na kushusha kiwango cha mavuno na ubora.
Kwa upande wake Mtafiti kutoka ICIPE Dkt. Shepard Ndlela amesema kupitia njia husishi za kudhibiti visumbufu mkulima ataweza kupunguza gharama na matumizi ya viuadudu vya kemikali na kuongeza mavuno na ubora kwa soko ndani na kimataifa.

Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo,Mkulima wa machungwa wa Kijiji cha Mkinga Wilaya ya Muheza mkoani Tanga Fatuma Muhammed amesema mafunzo hayo yamewasaidia sio tu kutambua wadudu waharibifu bali pia kutambua wadudu rafiki kwenye uzalishjai wa matunda ambao awali walidhani ni hatarishi lakini Wataalamu wamewaeleza ni wadudu rafiki wanaozuia wadudu waharibifu kushambulia matunda na wanachangia kuongeza tija.
“Sisi tulijua hawa wadudu (jamii ya siafu) tunawaita huku kwetu “madadada” kuwa ni waharibifu wa machungwa lakini wataalamu wametueleza ni wadudu rafiki wanaozuia wadudu wengine kushambulia machungwa” amesema Mohammed
Mafunzo hayo yamefanyika katika Wilaya za Hai, na Siha Mkoa Kilimanjaro na Muheza, mkoani Tanga ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa njia husishi za kudhibiti wadudu wa miti ya matunda kwenye ikolojia mbalimbali (Fruit tree agro ecological-based IPM).
Katika Wilaya za Hai na Siha mafunzo hayo yalijikita katika matunda ya parachichi, huku kwa Wilaya ya Muheza yakijikita kwenye matunda ya machungwa na embe.
Mradi wa ‘Fruit tree agro ecological-based IPM’ unatekelezwa kwa miaka mitatu (2023-2026) kupitia kituo cha TARI Ukiriguru kwa kushirikiana na Taasisi ya ICIPE chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).




Discussion about this post