NA MWANDISHI WETU,ARUSHA
MAMLAKA ya Rufani ya Zabuni za Umma Tanzania (PPAA) imejipanda kutoa elimu kwa wazabuni katika kanda zote nchini ikiwa ni jitihada za kuwafikia wadau wa ununuzi wa umma hususan wazabuni
Hayo yamezungumzwa mbele ya waandishi wa habari Septemba 12,2024 jijini Arusha pembezoni mwa Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki na Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA),James Sando
Sando amesema Mamlaka imeweka mkakati huo ili kuweza kuzifikia kanda nne ambazo hazijapatiwa elimu ya jinsi ya kuwasilisha mashauri yao pale ambapo hawakuridhishwa na mchakato wa ununuzi.
“Mkakati tulio nao katika mwaka huu wa fedha 2024/25 ni kuhakikisha kuwa tuwafikia wazabuni katika kanda nne ambazo hatujazifikia, katika kufika kwetu katika Kanda hizo tutakuwa tumewafikia wazabuni wengi,” amesema Sando
Sando amezitaja Kanda hizo kuwa ni Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kusini.
Wakati huohuo, Naibu Katibu Mtendaji wa PPAA, Florida Mapunda amezitaja faida za kuanzishwa kwa moduli ya kuwasilisha rufaa/malalamiko kwa njia ya kieletroniki na kueleza kuwa imesaidia kupunguza gharama na muda.
“Moduli hii itasaidia kupunguza gharama na muda kwa kuwa utaratibu wa zamani ulikuwa unamlazimu mzabuni kuwasilisha malalamiko yake katika ofisi za Mamlaka ya Rufani,”ameongeza Mapunda
Aidha amebainisha kuwa Moduli hii itamwezesha mzabuni au mfanyabiasha kuona hatua kwa hatua jinsi rufaa yake inavyoshughulikiwa hadi utoaji wa hukumu na kuongeza kuwa italeta uwazi na uwajibikaji na hivyo kuwapa imani wazabuni ya kuamini katika mifumo ya utoaji haki kwenye michakato ya zabuni za umma.
Kongamano la Wadau wa Ununuzi wa Umma limewakutanisha wadau wa ununuzi wa ndani ya Tanzania na Nje zaidi ya 1,500. Kauli mbiu ya kongamano hilo ni: “Matumizi ya Dijitali kwa Ununuzi wa Umma Endelevu.




Discussion about this post