• About
  • Advertise
  • Privacy & Policy
  • Contact
Thursday, January 22, 2026
  • Login
Bajeti
  • Home
  • Habari
  • Siasa
  • Mazingira
  • Magazeti
  • Makala
  • Picha
  • Michezo
  • Matangazo
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Siasa
  • Mazingira
  • Magazeti
  • Makala
  • Picha
  • Michezo
  • Matangazo
No Result
View All Result
Bajeti
No Result
View All Result
Home Makala

Kuelekea Siku ya Mbolea Duniani:Mazingira wezeshi yawa chachu ukuaji Tasnia ya Mbolea

by bajeti
September 30, 2024
in Makala
0
Kuelekea Siku ya Mbolea Duniani:Mazingira wezeshi yawa chachu ukuaji Tasnia ya Mbolea

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Joel Laurent (kulia) akipokea kishikwambi kutoka kwa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati wa hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vishikwambi na POS kwa Maafisa Ugani na Mawakala wa Pembejeo za Kilimo vitakavyorahisha usajili wa wakulima, iliyofanyika hivi karibuni jijini Dodoma.(Picha na TFRA)

Share on FacebookShare on Twitter

NA MWANDISHI WETU, TFRA

TANZANIA imeanza shamra shamra za kusheherekea Siku ya Mbolea Duniani inayoadhimishwa ifikapo Oktoba 13 ya kila mwaka .

Sherehe hizo ambazo mwaka huu wa 2024 zitafanyika kitaifa mkoani Manyara ambako wadau wote wa kilimo watakusanyika kuadhimisha siku hiyo.

Katika Jiji la Dodoma wataalam wabobezi wa masuala ya mbolea pamoja na watunga sera, watoa maamuzi, wafanyabiashara na wakulima watakusanyika ifikapo Oktoba 11 na 12,2024 kuhudhuria kongamano la aina yake na kuzungumzia mada mbalimbali ikiwemo matumizi ya mbolea katika kuhakikisha usalama wa chakula,

Hii ni siku inayoadhimishwa kama kumbukizi ya uvumbuzi wa kirutubishi kinachopatikana hewani  aina ya Amonia uliofanywa mwaka 1908 na Mwanasayansi  wa Ujerumani, Fritz Haber, kwa lengo la kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea.

Watanzania watasherehekea siku hii wakifurahia utashi wa kisiasa ulivyochangia  kuwepo kwa mazingira wezeshi ambayo yamesaidia ukuaji wa Sekta ya Mbolea nchini katika kipindi cha miaka mitatu chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mapema mwaka 2021, Rais  Dkt.Samia alipoingia madarakani, Serikali yake ilibuni mpango kabambe wa kutoa Ruzuku ya Mbolea kwa wakulima ili kuimarisha Sekta ya Kilimo iweze kutoa mchango mkubwa katika Uchumi wa Taifa.

Mpango huo wa Mbolea ya Ruzuku sasa umeleta hamasa kubwa miongoni mwa wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali  na hiyo ni kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Tanzania (TFRA) mwaka wa 2023.

Ni katika kipindi hicho cha miaka mitatu cha Uongozi wa Rais Dkt.Samia,Tanzania imeshuhudia kasi ya ujenzi wa viwanda vya mbolea na visaidizi vyake  na hivyo kuchochea  ongezeko la upatikanaji wa mbolea nchini ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, anasema hadi kufikia Juni 30, 2024, viwanda vya mbolea nchini vilifikia 23 vilivyozalisha jumla ya tani 158,628 za mbolea.

Anasema kiwanda kipya cha ITRACOM kinaendelea na ujenzi, ambapo kimekamilisha usimikaji wa mitambo mitatu yenye uwezo wa kuzalisha tani 600,000 kwa mwaka na inatarajiwa ifikapo mwisho wa msimu 2024/2025 kitakuwa kimekamilisha usimikaji wa mitambo yake  mitano yenye uwezo wa kuzalisha tani 1,000,000 kwa mwaka.

Laurent anabainisha kuwa Kiwanda cha Minjingu kilichokuwa na uwezo wa kuzalisha tani 100,000 kwa mwaka, kinatarajia kuongeza uzalishaji wake hadi kufikia tani 300,000 kwa mwaka ifikapo mwisho wa msimu 2024/2025.

‘’TFRA kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imefanya uhamasishaji wa uwekezaji katika viwanda vya mbolea ambapo Kampuni ya ESSA GROUP – Indonesia imeingia makubaliano  na TIC, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na TFRA kwa ajili ya uwekezaji kwenye kiwanda cha kuzalisha mbolea ya Urea.

‘’Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mbolea wastani wa tani 1,000,000 kwa mwaka na kinatarajiwa kutoa ajira takribani watu 4,500’’anasema Laurent

ONGEZEKO BAJETI YA KILIMO

Katika kujenga Uchumi Jumuishi na Endelevu unaolenga kuwanufaisha mamilioni ya wakulima wa Tanzania, Serikali sasa imekuja na tiba mahsusi kwa kuongeza bajeti kwenye maeneo ya Umwagiliaji, Matumizi ya Mbolea, Usambazaji wa Mbegu Bora, Uimarishaji Huduma za Ugani na Uwekezaji katika miundombinu.

Nia ya Serikali, kwa mujibu wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuziwezesha Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili zitoe mchango mkubwa kwa Uchumi wa Taifa na kuwatajirisha wakulima waliojiajiri kwenye sekta hizo muhimu.

Kwa miongo mingi, Sekta ya Kilimo ambayo ndiyo mwajiri mkubwa wa Watanzania, imekuwa ikipangiwa bajeti isiyotosheleza katika utekelezaji wa shughuli zake.

Hata, hivyo chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Mwaka 2023/2024 bajeti ya wizara ilikuwa Sh. Bilioni 970.8 ambayo sasa imepanda hadi kufikia Sh.Trilioni 1.248 kwa mwaka 2024/2025.

Juhudi za Rais  Dkt.Samia za kutoa kipaumble katika uendelezaji wa Sekta ya Kilimo,zimeongeza hamasa kwa wadau wa kilimo kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.

Katika kuhakikisha Wafugaji na Wavuvi wananufaika na uwekezaji na azma ya Serikali ya kuwaondoa kwenye umasikini, Rais Dkt. Samia anasema Serikali katika eneo la ujenzi na ukarabati wa viwanda vya mazao ya mifugo na miundombinu ya uvuvi vitapewa kipaumble.

Akihutubia kwenye kilele cha Maonyesho ya Nanenane jijini Dodoma Agosti 8,2024  Rais Dkt.Samia anasema lengo ni kuwasaidia Wafugaji na Wavuvi kupata mikopo yenye masharti nafuu kutoka vyombo vya fedha ili kuendeleza shughuli zao.

“Lengo la kujenga uchumi jumuishi ni kuongeza tija katika sekta za uzalishaji na kupunguza umasikini wa kipato cha mwananchi mmoja mmoja na kutumia Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutengeneza ajira,” ameeleza Rais  Dkt Samia .

Mwaka 2024/2025 Wizara ya Kilimo imepanga kuanzisha vituo 10 jumuishi vya kuhifadhi na kutoa huduma ya zana za kilimo kwa wakulima katika mikoa ya Dodoma, Njombe, Rukwa Mwanza, Mara, Iringa, Katavi, Singida, Manyara na Mbeya.

Kupanda kwa Bajeti ya Kilimo ni kuonyesha msukumo mkubwa uliowekwa na Serikali katika kuimarisha sekta hiyo ambayo inaajiri asilimia 75 ya Watanzania, hasa maeneo ya vijijini, anaeleza Mkurugenzi wa TFRA, Joel Laurent.

Mafanikio hayo ya TFRA yakijumuishwa na ujenzi wa maabara ya kisasa ya uchambuzi wa mbolea jijini Dar es Salaam ni jitihada za makusudi za Serikali za kutatua changamoto mbalimbali kwenye tasnia ya mbolea na kutengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji.

Kaimu Mkurugenzi Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja wa TFRA, Louis Kasera, anakiri  kwamba Serikali imefanya kazi kubwa kuweka mazingira wezeshi katika kila sekta ya kiuchumi, ikiwemo Sekta ya Mbolea, ili kuwavuta wawekezaji wa nje na wa ndani kuchangamkia fursa zilizopo katika tasnia hiyo.

Kasera anaeleza kwamba moja ya kichocheo kikubwa katika tasnia ya mbolea ni upatikanaji wa malighafi za viwanda kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea.

Malighafi hizo ni pamoja na madini ya Fosfeti, Gesi Asilia zinazofikia tani za ujazo trilioni 57, uwepo wa Makaa ya Mawe ya kutosha, Madini ya Chokaa na madini mengine yanayohitajika ambayo yametawanyika katika maeneo mbalimbali nchini.

Rais Dkt.Samia na viongozi waandamizi katika Wizara ya Kilimo na taasisi zake wanaamini kwamba Tanzania ni nchi iliyojaliwa kwa fursa za uwekezaji katika viwanda vya mbolea kwa sababu ni taifa lililozungukwa na soko kubwa la nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara lenye idadi ya watu zaidi milioni 600.

Kwa mujibu wa takwimu za TFRA asilimia 90 ya mbolea zinazotumika Tanzania zinaagizwa kutoka nje wakati kiasi kilichobaki cha asilimia 10 ndicho kinachozalishwa na viwanda 15 vilivyopo nchini kwa sasa.

Azma ya Serikali ni kuona kwamba Tanzania inajenga mazingira ya kujitosheleza kwa pembejeo kama mbolea ili kuepuka uagizaji kutoka nje – hasa kutokana na gharama za matumizi ya fedha za kigeni.

Kiwanda cha Minjingu kilichopo mkoani Manyara ndicho kikubwa zaidi ambacho kinazalisha asilimia 80 ya visaidizi vya mbolea.

Viwanda vingine vinavyozalisha visaidizi vya mbolea ni ABM Equipment kilichopo Tanga na Dodoma Cement cha Jiji la Dodoma ambapo vingine ni Kahela Traders, Keen Feeders Co. Limited, Sianga Agro Trade Company, Mtali Agrotraders and Amka Feeder’s, ambavyo vyote hutengeneza mbolea za majimaji.

Baadhi ya wafanyabiashara wa mbolea Kanda ya Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuhitimu mafunzo ya biashara ya mbolea yaliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) katika ukumbi wa Manisapaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam hivi karibuni.(Picha na TFRA)

FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA MBOLEA

Kwa kuwa mbolea zinazozalishwa nchini hazikidhi mahitaji, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia imelazimika kubeba jukumu la kuwavuta wawekezaji nchini ili kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea.

Fursa za uwekezaji zilizopo kwenye tasnia ya mbolea ni pamoja na utashi wa kisiasa na mazingira wezeshi, uwepo wa soko la ndani na nje lakini pia bila ya kuwepo kwa utashi wa kisiasa ni vigumu kwa nchi yoyote duniani inayoweza kufikia Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu.

Kwa Tanzania, inayojivunia eneo lake la kijiografia, lipo soko kubwa la mbolea kwenye nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Maendeleo wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

MIUNDOMBINU THABITI SEKTA YA UCHUKUZI

Hivi sasa Tanzania inajivunia kuwepo kwa ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya barabara na reli kwa ili kuimarisha Sekta ya Uchukuzi.

Kwa sasa zaidi ya asilimia 70 ya eneo la Tanzania  liinapitika kwa barabara za lami, ukiacha ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayoendelea kujengwa kutoka Jiji la Kibiashara la Dar es Salaam kwenda nchi jirani za Afrika Mashariki kama vile Rwanda,Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo(DRC)

USALAMA WA CHAKULA

Uamuzi wa Serikali ya Tanzania kuweka msukumo mkubwa katika Tasnia ya Mbolea ni kuimarisha usalama wa chakula kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu la asilimia 4.8 kila mwaka ambapo kwa mujibu wa Sensa  ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022)  Tanzania ina watu Milioni 63, lakini pia kuongeza malighafi viwandani.

Katika miaka mitatu ya uongozi wake, Rais Dkt.Samia amekuwa akiwahimiza watendaji wa ngazi zote kusimamia kikamilifu mageuzi yanayofanyika katika Sekta ya Kilimo ili sekta hiyo itoe mchango wake kwa Uchumi wa Taifa.

Rais Dkt.Samia amekuwa akisisitiza kwamba maamuzi ya Serikali kutoa Ruzuku ya Mbolea kwa wakulima ni kuwawezesha kutumia fursa hiyo kuzalisha kibiashara ili kupata chakula cha kutosha pamoja na ziada ya kuuzwa nje ya nchi na kuingiza fedha za kigeni.

KUANZISHWA MFUKO WA PEMBEJEO

Hata hivyo Rais Dkt.Samia kila wakati amekuwa akisisitiza kwamba ongezeko la uzalishaji mashambani litaifanya Serikali  kuanzisha Mfuko wa Pembejeo utakaotumika wakati wa dharura, hasa kunapotokea kupanda kwa bei za Pembejeo za Kilimo.

Mipango mahsusi ya Serikali ya kuongeza uzalishaji wa mbolea nchini ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha Itracom Fertilizer Limited kilichopo Dodoma  na upanuzi wa kiwanda cha Minjingu mkoani Manyara, ambavyo vyote vitapunguza adha wanayopata wakulima wa kununua mbolea kwa bei kubwa.

Miaka mitatu ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia imeshuhudia Serikali yake ikijitahidi  kuvijengea uwezo viwanda vya mbolea vya ndani na kumjengea uwezo mwekezaji mkubwa wa kiwanda cha mbolea cha Minjingu aweze kupata mikopo itakayomsaidia kuendeleza kiwanda hicho ili kuongeza uzalishaji.

Hakuna ubishi kuwa kwa miongo mingi ijayo, kilimo kitaendelea kuwa ni Uti wa Mgongo wa Tanzania kutokana na ukweli kwamba sekta hiyo ndiyo mwajiri mkubwa wa asilimia 75 ya Watanzania wote.

Ndiyo maana tangu Tanzania Bara ipate uhuru wake kutoka Waingereza zaidi ya miaka 60 iliyopita Serikali za awamu zote zimekuwa zikitilia mkazo sekta hiyo.

Kampeni inayoendelea nchini kuhusu matumizi ya mbolea kwenye kilimo imehusisha wadau wengi kuanzia wizara mama ya Kilimo, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, Sekretarieti za mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Waingizaji/Wazalishaji wa Mbolea, Mawakala  wa Mbolea, Taasisi za Fedha na za kulima.

Wadau hawa wamehusishwa ili kuhakikisha kwamba kampeni hii ya matumizi ya mbolea katika kilimo haikwami mahali popote na nia ni kuhakikisha mbolea inamfikia mkulima kwa njia rahisi na kwa bei iliyopangwa na Serikali badala ya kupitia njia zisizo halali kama vile ulanguzi wa bidhaa hiyo.

WAZIRI BASHE NA KILIMO CHA KISASA

Hussein Mohamed Bashe, Waziri wa Kilimo amekuwa ni mhimili mkubwa wa kusimamia kikamilifu suala la matumizi ya mbolea nchini kote.

Zipo taarifa za kutia moyo kwamba katika mikoa mingi nchini matumizi ya mbolea sasa yamezaa matunda kwa kuchochea ongezeko la uzalishaji.

Miaka mitatu ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia imeshuhudia ongezeko la matumizi ya mbolea katika kilimo na kuwapa matumaini wakulima ya kubadilika kwa hali zao za maisha siyo tu kiuchumi bali pia kujitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada ya kuuza.

Kwa miongo kadhaa baada ya uhuru, baadhi ya wasomi walikuwa wakikiona kilimo kama ni adhabu au mateso kwa sababu kilikuwa kikionekana hakina tija kwa wakulima.

WASOMI WAKIMBILIA KILIMO

Baadhi ya Vijana waliofuzu mafunzo ya uendeshaji wa biashara ya mbolea wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorrow – BBT) wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent hayupo (pichani) kabla ya kutunukiwa vyeti na Mamlaka hiyo wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma Septemba 22,2024.(Picha na TFRA)

Kwa Tanzania ya leo, vijana wengi wasomi wameanza kukimbilia kilimo kama chanzo cha asali na maziwa.

Katika Ulimwengu huu wa ukosefu wa ajira, vijana wasomi sasa wameanza kugeuka wakulima hodari wa mazao mbalimbali ya Biashara na Chakula.

Msukumo wa Serikali ya Awamu ya Sita kuhusu Tasnia ya Mbolea umesaidia kuwaelimisha wakulima na wadau mbalimbali kwamba “Kilimo Kinalipa” kwa watu ambao ni makini katika kujiletea utajiri.

Hamasa ya Rais Dkt. Samia kuhusu ujenzi wa viwanda vya mbolea imezaa matokeo chanya ya upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu, na hivyo kuongeza uzalishaji, usalama wa chakula, kudhibiti mfumuko wa bei za vyakula na kuinua kipato cha mkulima.

Next Post
Dkt.Biteko awataka wazazi na walimu kuwaandaa wanafunzi kuwa viongozi bora wa siku zijazo

Dkt.Biteko awataka wazazi na walimu kuwaandaa wanafunzi kuwa viongozi bora wa siku zijazo

Kuelekea Siku ya Mbolea Duniani, ni wakati mzuri wa kuelewa dhana ya matumizi sahihi ya mbolea

Kuelekea Siku ya Mbolea Duniani, ni wakati mzuri wa kuelewa dhana ya matumizi sahihi ya mbolea

TFRA yanadi fursa Tasnia ya Mbolea Oman

TFRA yanadi fursa Tasnia ya Mbolea Oman

Discussion about this post

Contact us:

BAJETI COMMUNICATION

info@bajeti.co.tz
bajetinews@gmail.com
+255718699828
P.o.BOX 18133,
DAR ES SALAAM,
TANZANIA

Category

  • Habari
  • Magazeti
  • Makala
  • Mazingira
  • Michezo
  • Picha
  • Sayansi na Teknolojia
  • Siasa

Our Visitors

  • Today's visitors:18
  • Today's page views 18
  • Total visitors 13,277
  • Total page views 15,025

Kuhusu Tovuti Hii

Hii ni tovuti ya habari iliyojikita katika kuandika  habari za kina   zikiwemo za mazingira kwa lengo la kuelimisha na kuuhabarisha umma.

Subscribe

  • About
  • Advertise
  • Privacy & Policy
  • Contact

© 2025 Bajeti

No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Siasa
  • Mazingira
  • Magazeti
  • Makala
  • Picha
  • Michezo
  • Matangazo

© 2025 Bajeti

Welcome Back!

Login to your account below

Forgotten Password?

Retrieve your password

Please enter your username or email address to reset your password.

Log In