NA MWANDISHI WETU,TFRA
TUNAPOELEKEA kuadhimisha Siku ya Mbolea Duniani mwaka huu wa 2024, ni wakati mzuri kwa wadau mbalimbali wa Tasnia ya Kilimo, wakiwemo wakulima kama walengwa, wa kuielewa dhana ya matumizi sahihi ya mbolea.
Kwa baadhi ya wakulima dhana hii imekuwa ikipewa tafsiri nyingi ambazo huwakanganya kutokana na kubeba maana pana.
Ndiyo maana kuanzia Oktoba 10 hadi 13 kuelekea kilele cha Siku ya Mbolea Duniani, wananchi wa mkoa wa Manyara watapata fursa nzuri ya kupata maelezo fasaha kutoka kwa wataalam.

kuu la kuhifadhia mbolea la kampuni ya ETG lilipo Ungalimited jijini Arusha.
Meneja wa Ukaguzi wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) na Mtaalam Mbobezi wa Udongo, Dkt Asheri Kalala, anaeleza kwamba upo uhusiano mkubwa kati ya mbolea na udongo kwa kilimo endelevu.
“Kwa kawaida tunatakiwa kuweka mbolea kulingana na mahitaji ya mmea ikiwemo kiasi kamili kinachotakiwa kwa mmea kwani kila aina ya zao lina mahitaji tofauti na tunajua hili baada ya kupima udongo,” anaeleza.
“Kwa ujumla zao la mahindi, hasa mbegu chotara ili kuzalisha tani moja zinahitaji kilo 27, 7.5, na 20 za naitrojeni, fosforasi na potasiumu, mtawalia na hii inamaanisha kwamba tani tano za mahindi zinahitaji sawa na kilo 135 za naitrojeni, 37.5 za potasiumu na kilo 100 za kalisiumu kwa hekta moja.”
TUNAJUAJE MAHITAJI YA MBOLEA?
Anasema kwa kawaida wakiona dalili za upungufu wa kirutubishi kukosekana kwenye mmea wanakuwa tayari wamechelewa,
Hivyo historia ya uzalishaji kwa misimu iliyopita inaweza kuwaelekeza kuwa virutubishi kadhaa vinapungua kwenye udongo na vinahitaji kuongezwa kupitia mbolea ambapo kila mmea unatoa dalili fulani kuashiria upungufu wa virutubisho husika.
Kwa ujumla kwenye mahindi naitrojeni inahitajika kufanya mmea ukue kwa kasi; majani yanakuwa ya kijani kilichoiva na huandaa mmea kuweka mbegu za kutosha na ikipungua majani hubadilika kuwa ya njano, shina huwa dogo na mhindi kuwa mdogo.
Fosiforasi hufanya mizizi ya zao kuwa na nguvu na kuweza kujiimarisha kwa kuchukua virutubisho vingine toka kwenye udongo kwa ajili ya utengenezaji sukari mbalimbali zinazohitajika kwa ukuuaji na kutengeeneza Punje ambapo Potasiumu ikikosekana majani ya muhindi hugeuka zambarau, shina huwa dogo na mmea hukua taratibu.
Hali hii husababisha kutojaa kwa mistari kwenye muhindi na uzalishaji hafifu.Potasiumu (K) ni muhimu kwa kutengeneza sukari, protini na inahusika kusafirisha chakula kilichotengenezwa kwenye majani kufanyika kuwa mbegu ambapo nayo huimarisha mmea kuwa shina kubwa, muhindi kuwa mkubwa na huongeza uimara mmea kutoshambuliwa na magonjwa.
Ukosekanaji wa potasiumu kwenye udongo husababisha mmea kuwa mfupi, mbegu chache, na mbegu huwa nyepesi ambapo Virutubishi hivyo ni muhimu na vinahitajika muda wote vipatikane kwa wingi kwa uzalishaji wenye tija.
Mbolea humaanisha kitu chochote aidha cha kikemikali au cha asili ambacho hutumika kuupatia virutubisho mmea, ikiwa kupitia kwenye udongo, au majani, au kwenye maji (mpunga) au mchanganyiko wa maji na virutubisho (fertigation na hydroponinics).
Chanzo cha virutubisho chaweza kuwa kikemikali na mbolea za viwandani, mboji (organic) kama samadi kutokana na mifugo, maozea (composts), makusanyo ya maji machafu (sludges) na mabaki mengine ya vitu
mbalimbali.
KWANINI TUNATUMIA MBOLEA?
Kitaalamu, ili mmea ukue vizuri unahitaji virutubisho 17 ambapo vitatu kati ya hivyo (C, H, O) hutoka kwenye maji na hewa na vilivyobaki 14 hutoka kwenye udongo unaozunguka mmea unapoishi. Virutubishi sita kati ya 14 vinavyopitia kwenye udongo huhitajika kwa kiwango kikubwa (macronutrients) vikiwemo naitrojeni, fosforasi, potasiumu, salfa, kalsiumu, na maginesiumu ( kwa ufupi N, P, K, S, Ca, na Mg).
Virutubishi vilivyobaki vinane vinahitajika kwa uchache (micronutrients) boroni, klorini, shaba, chuma, manganisi, molibdenamu, nikeli, na zinki (B, Cl, Cu, Fe, Mn, Mo,,Ni, na Zn) navyo ni muhimu kuwepo.
Virutubisho hivyo havipatikani kwa utoshelevu kwenye udongo ndio maana tunaweka mbolea ili kufanya vipatikane kwa kiwangokinachotakiwa.
Mbolea huwekwa kwenye udongo vipindi tofauti vya mmea kukua kwa kuzingatia wakati wa kupanda, kukuzia ama kuzalishia.
Kwa kawaida wakati wa kupanda fosiforasi huhitajika kwa wingi na naitrojeni kiasi kidogo ili kuupa mmea mizizi kuimarika (DAP na NPK zenye P nyingi huwekwa wakati huu). Wakati wa kukua kwa haraka (vegetative) N huhitajika kwa wingi na ndio wakati kama huu mbolea kama CAN, Urea, SA hutumika.
Hii hutengeneza mjengeko mzuri wa mmea (vigorous) na kukusanya chakula cha kutosha kwa ajili ya kuzaa.
.Kupima udongo kwa ajili ya matumizi ili kuwa na uhakika wa kiasi kamili cha virutubisho vinavyohitajika tunahitaji kupima udongo.
Udongo hupimwa kwenye maabara na kubaini uwingi wa virutubishi vilivyopo kwenye udongo husika. Taarifa za maabara (data) hutumika na wataaalamu kukokotoa kiasi cha kirutubishi kinachotakiwa au vifaaa vya kisasa hutoa makadirio ya moja kwa moja virutubisho vinavyohitajika.
Kuna vitu kadhaa vikipimwa kwenye udongo huashiria viwango vya mbolea vinavyotakiwa.
Kipimo cha tindikali au pH na ukaa (carbon) huashiria afya ya udongo na virutubishi vinavyoweza kuwa vinapungua au kutosheleza. Udongo wenye pH ndogo haswa chini ya 5.5 husemeakana kuwa ni acidic soils na huhitaji kupandishwa ili virutubishi vilivyotajwa hapo juu viweze kuchukuliwa kwa usahihi.
pH ikiwa ya juu sana kuanzia 8.5 udongo husemekana kuwa wa chumvi/magadi na mazao yake huwa hafifu.
Kurekebisha hali hizo udongo wenye tindikali huhitaji kuwekewa chokaa kilimo ili kuongeza pH na udongo wenye alkali huwekewa jasi au gypsum kupunguza pH na kawaida mimea mingi hukua vizuri kwenye pH 6.0 mpaka 7.5.
Matumizi sahihi ya mbolea na uhusiano wake na ubora wa chakula
Matumizi ya mbolea sahihi yanatakiwa kufuata mbinu nzuri kwa kuhakikisha muda wote wa zao likiwa shambani linapata virutubishi vya kutosha kwa muda sahihi kwa kufuata (4R stewardship) ambazo ni chanzo sahihi (the Right Source of nutrients); kiasi sahihi (Right Rate); wakati sahihi (Right Time) na mahali sahihi (Right Place).
Kuainisha huu utaratibu na kuufuata huwa na matokeo chanya kwa kutoa mazao yenye faida na kuzuia uharibifu katika mazingira.
Mimea iliyopata virutubisho hutoa uhakika wa chakula ambacho kina madini na virutubisho toshelezi, ikihusisha kuimarisha afya ya binadamu atakayokitumia.
Matumizi sahihi ya mbolea za mboji, na za viwandani zitasabisha ulinganifu wa matumizi ya virutubishi na kusababisha uzalishaji ulio bora
Athari za matumizi ya mbolea yasiyo sahihi
Huzalisha mawazo potofu za kufikiri matumizi ya mbolea za viwandani husabaisha udongo kuharibika. Virutubishi vyote 17 vinahitajika kuwepo wakati wote wa mmea kukua, ikitokea kirutubishi kimojawapo kikipungua husababisha muonekano hafifu wa mazao na uzalishaji huwa mdogo na kusababisha na mkulima kufikiri udongo umeharibika.
Matumizi yasiyo sahihi husababisha mrundikano wa virutubisho visivyohitajika kwenye udongo na kuweza kusombwa kupelekwa kwenye vyanzo vya maji na kusababisha uharibifu wa mazingira kama kuota mimea kwenye mabonde, mito na maziwa.
Ili kilimo kiendelee kuchangia ukuaji wa uchumi na kuendelea kutoa ajira kwa wananchi walio wengi kwa kuwaongezea kipato chenye tija, wakulima wanatakiwa kutumia mbolea kwa usahihi kama wataalamu wanavyoelekeza.




Discussion about this post