NA MWANDISHI WETU,TFRA
OKTOBA 13, 2024 Tanzania itaungana na mataifa mengine Ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Mbolea Duniani, ambapo mchango wa vijana na wanawake katika kuimarisha biashara ya mbolea litakuwa moja ya maeneo yanayofanyiwa tathmini ya kina ili kuhamasisha harakati za kukuza sekta mama ya kilimo.
Katika kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani, madhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yametumika kwa wadau mbalimbali wa kilimo, wakiwemo vijana na wanawake, kutathmini mchango wa mbolea katika uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara.
Kupitia jukwaa hili la Siku ya Mbolea, Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Tanzania (TFRA) ni moja ya taasisi ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kuongeza ajira zenye staha na ushiriki wa vijana na wanawake kwenye kilimo.
Kwa kupitia Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), TFRA imetoa mafunzo ya elimu ya biashara ya mbolea kwa vijana na wanawake ikiwa ni mchango wake unaolenga kuongeza ajira za staha, kuongeza tija, kubakiza wakulima kwenye sekta na kupunguza umasikini.
Wakulima, Watunga Sera na Watoa Maamuzi wanapojiandaa kusheherekea Siku ya Mbolea Duniani wanalishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuanzisha Programu ya BBT ikiwa na malengo manne ya kuongeza ajira, mitaji, teknolojia na umilikishwaji wa ardhi.
Programu hiyo inatekelezwa kupitia miradi minne ambayo ni mashamba makubwa ya pamoja, utoaji wa mikopo yenye riba nafuu, visima kwa wakulima wadogo na ugani.
Programu hiyo ambayo inahesabika kama mkombozi kwa maelfu ya vijana na wanawake ilizinduliwa rasmi na Rais Dkt.Samia mwezi Machi mwaka 2023.
Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, hadi kufikia Aprili mwaka huu 2024, jumla ya ekari 340,465.28 zimeshapatikana kwa ajili ya programu ya BBT mikoa ya Dodoma, Kigoma, Mbeya, Singida, Pwani, Tanga, Njombe na Kagera.
Katika kuimarisha ushiriki wa vijana na wanawake katika programu hii, Wizara ya Kilimo imetoa mafunzo kuhusu kilimo biashara na kuwapatia mashamba.
Ni katika programu hii ya mafunzo ya elimu biashara ya mbolea,Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, hivi karibuni aliwakabidhi vyetu vijana 192 wa BBT waliohitimu mafunzo hayo.
Mafunzo ya vijana hao yalifanyika katika shamba lao la Chinangali II wilayani Chamwino, Mkoa Dodoma.
Vyeti walivyokabidhiwa vijana hao vitawasaidia kujisajili kuwa mawakala wa pembejeo za mbolea ambapo jumla ya ekari 5,700 kati ya ekari 11,430 katika shamba la Mlazo/Ndogowe zimesafishwa na visima 12 na mabwawa matano yamechimbwa kwa ajili ya kuhifadhi maji ya umwagiliaji.
Mbali na hilo lakini pia jumla ya ekari 1,000 katika shamba hilo zimetengwa kwa ajili ya kuwapatia wanakijiji wanaolima kulizunguka shamba hilo.
Hali kadhalika, nyumba 53 zimejengwa katika shamba hilo kwa ajili ya vijana na wanawake wa BBT.
Kwa kutambua umuhimu wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo, TFRA iliratibu mafunzo kwa vijana 192 kwa kushirikiana na Idara ya Mafunzo ya Wizara ya Kilimo kupitia Vyuo Vya Mafunzo (MATI) ili kutoa mafunzo ya uendeshaji wa biashara ya mbolea kwa kuzingatia Sheria ya Mbolea Na. 9 ya mwaka 2009.

Akizungumza na vijana hao wakati wa zoezi la ugawaji vyeti,Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Joel Laurent anasema matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka 500,000 kwa mwaka 2022/2023 hadi kufikia tani 840,000 mwaka 2023/2024.
Anasema Ongezeko hilo lilichagizwa na ruzuku ya mbolea iliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
“Ongezeko la matumizi ya mbolea ni kubwa; hii inaashiria namna jamii ilivyoelimika na kutambua umuhimu kwenye shughuli za kilimo,” anasema na kuendelea: “ TFRA inaendelea kupanua wigo wa utoaji elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima ili waendelee kunufaika.”anaongeza Laurent
Laurent anawapongeza vijana waliomaliza mafunzo yao kwa kuwa yatawajenga katika Sekta ya Kilimo waliyoichagua kama nguzo ya uchumi wao.
Aidha anabainisha kuwa mafunzo yaliyotolewa kwao yana maana zaidi kwa maandalizi ya msimu ujao wa kilimo wa 2024/2025.
Mkurugenzi huyo wa TFRA pia ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuwalea vijana wa BBT, hatua ambayo inasaidia katika ukuaji wa sekta mama ya kilimo.
Naye Mratibu wa Mradi wa BBT, Mathed Kahaya, anaishukuru TFRA kwa kutoa mafunzo hayo kwa vijana akisema ni lazima wayazingatie ili waweze kunufaika katika shughuli zao za kilimo.




Discussion about this post