NA MWANDISHI WETU,TANGA
SERIKALI inaandaa mpango wa kuongeza misitu ya asili kwa kila halmashauri nchini kuwa na msitu wake ikiwa moja ya njia ya Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira utakaosaidia katika biashara ya kaboni.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji ameyasema hayo Oktoba 23,2024 wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo.
Dkt. Kijaji ameeleza kuwa lengo ni halmashauri hizo ni kuingia kwenye biashara ya Kaboni ambapo zoezi la kupandwa miti kwa pamoja litawezesha faida kuonekana haraka kuliko kupandwa na mtu mmoja mmoja.
Aidha ameongeza mpango huo utashirikisha hasa wale ambao wana maeneo makubwa ya ardhi ambapo wanaweza kutumia ekari tano hadi 10 kwa ajili ya kupanda miti hiyo.
“Kufanikiwa kwa kupandwa miti hiyo kutasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo mengine yanasababisha ongezeko la joto pamoja na mvua ambazo hazina mpangilio mzuri,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amesema kumekuwepo na changamoto ya wananchi kuchoma misitu hovyo na hivyo wamekuwa wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi kuona jinsi ya kuzuia matukio hayo.
Ameeleza kuwa mkoa huo una zaidi ya hekta 700,000 za misitu ambapo ndani yake kuna mashamba matatu ya miti lakini kumekuwa na changamoto ya wananchi kuvamia na kuingiza mifugo pamoja na kuchoma mkaa, ambapo mamlaka husika zinaendelea na udhibiti.
Amesisitiza kuwa katika mkoa huo wananchi pia wamekuwa wakijishughurisha na kilimo cha mikoko ambacho kinasaidia katika utunzaji wa mazingira ya bahari kwani wakati wa mmomonyoko wa udongo miti hiyo inasaidia kusitokee uharibifu kwenye maeneo ambapo mikoko ipo.




Discussion about this post