NA MWANDISHI WETU
AFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Godfrey Nyaisa amesema Taasisi hiyo kwa sasa imetekelea agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan juu ya kuhakikisha Mifumo yote ya Kitaasisi inasomana.
Nyaisa ametoa kauli hiyo Oktoba 25,2024 mkoani Dar es Salaam katika ufunguzi wa mkutano wa pili wa Taasisi hiyo na wadau wake.
Amesema lengo ni kurahisisha utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao na kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara kwa ujumla.
‘’Urasimishaji wa biashara ni mchakato kwa maana ya “process”,Usajili aidha wa Kampuni au Jina la Biashara ni sehemu ya mchakato tu wa Urasimishaji wa biashara.
‘’Mara baada ya kusajili Mfanyabiashara anatakiwa kupata leseni au vibali kutoka Mamlaka nyingine za Serikali ikiwa ni pamoja na Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), Leseni ya Biashara na Vibali kutoka Mamlaka za Uthibiti “Regulatory Authorities”amesema Nyaisa
Amesema kwa namna ya kipekee ametambua uwepo wa Taasisi dada kutoka upande wa Zanzibar; Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) wanaotoa huduma sawa na BRELA, na Ofisi ya Hakimiliki Zanzibar (COSOZA) wanaotoa huduma sawa na COSOTA.
‘’Uwepo wa Taasisi za Umma na Binafsi kwenye Mkutano huu wa pili wa BRELA na wadau wake utasaidia kujadili mafanikio, fursa na changamoto za Sekta ya Biashara.
‘’Kauli Mbiu ya Mkutano wa Mwaka huu ni “Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini” (Interoperability of Institutional Systems and Business Facilitation),wote ni mashaidi kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mpendwa Samia Suluhu Hassan, amekuwa akitoa maelekezo na miongozo ya Mifumo ya Taasisi za Serikali kusomana.
‘’Lengo ni kurahisisha utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao na kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara kwa ujumla’’amefafanuwa Nyaisa
Aidha ameongeza kuwa mageuzi makubwa yalianza kufanyika Desemba 3, 1999, baada ya BRELA kuwa Wakala wa Serikali chini ya Sheria ya Wakala za Serikali “Executive Agency Act No. 30 of 1997” ambapo mabadiliko haya yalilenga kuharakisha utoaji huduma na kuboresha mazingira ya utendaji kazi.
‘’Mwaka 2015 BRELA ilianzisha mfumo wa kwanza wa usajili wa Majina ya Biashara kwa njia ya Mtandao “Online Business Name Registration System – OBRS” ambapo mfumo huo ulitengenezwa na watumishi wa BRELA kwa kushirikiana na vijana wengine wakitanzania na Januari 4, 2018, BRELA ilianza kutumia mfumo mpya wa Usajili kwa Njia ya Mtandao “Online Registration System- ORS”, mfumo huu unatoa huduma zote za sajili na za baada ya sajili “Registration and Post Registration” zikiwa ni pamoja na sajili za Makampuni, Majina ya Biashara, Alama za Biashara na Huduma, Hataza pamoja na Leseni za Viwanda.
‘’Kwa upande wa Leseni za Biashara za Kundi “A” zilizohamishiwa BRELA kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara pia zinatolewa kwa njia ya Mtandao kupitia Mfumo wa “Tanzania National Business Portal – TNBP”.
‘’Huduma hizi zimerahisisha sana wateja kupata huduma popote pale walipo, huduma nyingine zikiwa ni kwa siku moja tu ambapo kabla ya mifumo hii kuanza wateja walikuwa wanalazimika kutoka sehemu zote za nchi kuja kupata huduma Dar es Salaam huku huduma nyingine zikigharimu kiasi cha Sh. 1,000 lakini wateja walilazimika kutoka Mbeya, Arusha, Mwanza, Rukwa na mikoa mengine kufuata huduma hii”amesema Nyaisa
Nyaisa ameeleza kuwa Mfumo huo wa ORS umetimiza miaka sita,na ni dhairi teknolojia na baadhi ya sheria zimebadilika sana.
‘’Hivyo, sisi kama BRELA tulishaanza maboresho ya Mfumo huo kwa kuufanya uwe bora na rafiki zaidi, nikiri kuwa katika mfumo wa sasa kuna baadhi ya taarifa zinazolazimu kujazwa zaidi ya mara moja, kitu ambacho mfumo ungeweza kuvuta taarifa hizo bila kuhitaji kujazwa tena. Zoezi la maboresho lilishirikisha maoni ya wadau kwani wao ndiyo watumiaji wakubwa wa Mfumo huu.
‘’Maboresho haya yamezingatia uwepo wa huduma zingine, mfano upande wa Leseni za Biashara, BRELA inaendelea na mashauriano na mamlaka zingine ili kutumia mfumo mmoja wa Leseni za Biashara utakao kuwa na uwezo wa kutoa Leseni za Kundi “A” zinazotolewa na BRELA na Leseni za Kundi “B” zinazotolewa na Serikali za Mitaa “Local Government Authorities” bila kuathiri mapato ya Halmashauri husika.’’amebainisha Nyaisa
Aidha Nyaisa ameishukuru Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kusimamia kwa dhati majadiliano ya kuwa na mfumo mmoja wa utoaji Leseni za Biashara na Uanzishwaji wa mfumo huo mmoja wa Leseni utaisaidia sana Serikali kwenye takwimu pamoja na kuthibiti upotevu wa mapato kwa kuondoa leseni za kuandikwa kwa mikono.



Discussion about this post