NA GOODLUCK HONGO,MTWARA
SERIKALI imeendelea kupeleka mabilioni ya fedha katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini-Mtwara (Mitengo) ambapo sasa mgonjwa haitaji kuwa na rufaa ili apate huduma za kibingwa za madaktari bingwa.
Mbali na hiyo lakini kwa sasa hospitali hiyo mpya inayohudumia mikoa ya Lindi,Mtwara na Ruvuma zikiwemo nchi jirani za Msumbuji na Visiwa vya Commoro ina uwezo wa kuotesha sampuli na kubaini vimelea na dawa gani ya kutibu vimelea hivyo

Akizungumza na Bajeti Communication Oktoba 28,2024 mkoani Mtwara waliotembelea hospitali hiyo kujionea uwekezaji wa Serikali uliofanyika katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya,Mkuu wa Kitengo cha Maabara katika hospitali hiyo, Shaibu Nanyanga amesema Serikali imetoa fedha nyingi katika kuboresha jengo la maabara,idara ya kemia hai na mikrobiolojia ambapo vitengo hicvyo vipo ndani ya jengo moja la maabara.
Amesema kiasi cha zaidi ya Sh.Milioni 240 zilizotolewa zimefanya uwekezaji mkubwa waa kitengo cha maabara kwa kununua mashine za kisasa na kwa upande wa idara ya kemia hai ambapo awali walikuwa wakitumia mashine ndogo hivyo kuwezesha kitengo hicho kupima sampuli za aina mbalimbali na kutoa majibu ya haraka..
‘’Kwa sasa tunauwezo wa kupima sampuli zaidi ya 600 kwa wakati mmoja na kutoa majibu kwa haraka kwa wateja wetu’’amesema Nanyanga

Akizungumzia uwekezaji uliofanyika upande wa Mikrobiolojia(Maabara ya kuoteshavimelea vinavyosababisha magonjwa katika mwili wa mwanadamu), Nanyanga amefafanua kuwa Serikali ilipeleka fedha kiasi cha Sh.Milioni 108 ili kuimarisha uwezo wa maabara hiyo ambapo kwa sasa inauwezo wa kuotesha sampuli zote za kibaiolojia ikiwemo mkojo,damu na vingine.
‘Idara ya Mikrobiolojia ni idara muhimu sana kwa utoaji huduma kwa wateja wetu na tunaamini kwa uwekezaji uliofanyika katika idara hii utaturahisishia kwa kiasi kikubwa kupambana na usugu wa madawa kwa mteja wetu’’
Akizungumzia uwekezaji mwingine,Nanyanga ameongeza kuwa mbali na hayo lakini pia sasa wana uwezo wa kutoa vipimo vya aleji,ambapo kwa kiasi kikubwa jamii inasumbuliwa na aleji tofautitofauti zikiwemo za vumbi,vyakula na vingine tofauti ambapo mteja anaweza kugundua aleji yake imesababishwa na nini.
‘’Tunauwezo wa kupima parameta 20 tofauti za aleji vikiwemo vyakula vya ngano na vingine’’anaeleza Nanyanga
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji na Daktari Bingwa wa Mifupa na Majeraha katika hospitali hiyo,Dk Lameck Moses amesema hivi karibuni wameongezewa huduma zingine katika ufanyaji wa upasuaji wa mifupa ikiwemo mifupa mirefu ya paja na ile ya chini ya goti.
Amesema Serikali imeongeza kasi ya uwekezaji katika hospitali hiyo ambapo kwa sasa mgonjwa haitaji kupata rufaa ili aweze kupata huduma za kibingwa kutoka kwa madaktari bingwa.

‘’Huduma za mifupa ambazo tunatoa za kibingwa ni zile za maumivu ya mifupa,maumivu ya viungio mbalimbali,huduma za kuvunjika au kupata majeraha mbalimbali ambayo yanatokana na aina mbalimbali za ajali hususani zile za barabarani na zile zinazotokana na mtu kujikata au kudondokewa na vitu au kuanguka mwenyewe wakati anatembea.
‘’Hivi karibuni tumeongezewa huduma mbalimbali ambapo mwanzoni baadhi ya mivunjiko au majeraha tu ndio tulikuwa tunahudumia lakini kwa uwekezaji mkubwa wa Serikali na baadhi ya vifaa ambavyo hospitali imewekeza imeongeza chachu ya mivunjiko mbalimbali katika ufanyaji wa oparesheni hasa upasuaji wa mifupa’’amesema Dk Moses
‘’Tunawaasa wananchi waendele kufika katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini kwa sababu hadi sasa hivi hatuhitaji uwe na rufaa ndipo uje ufanye huduma za kibingwa za madaktari bingwa wa mifupa na unaweza ukatokea tu nyumbani na ukafika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini na kisha ukamuona Daktari Bingwa wa upasuaji wa mifupa na akakupatia huduma kwa muda mfupi zaidi kama Serikali inavyoelekeza’’amesema Dk.Moses
Baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma katika hospitali hiyo wameeleza kufurahishwa kwao na kuishukuru Serikali ambapo uwepo wa huduma bora na za kisasa wanazopatiwa kwa utaratibu maalum na kwa wakati kumewafanya kujiona kama sio wagonjwa.

Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini Mtwara ilianza kazi Oktoba Mosi,2021 ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan aliifungua rasmi mnamo Septemba 15,2023



Discussion about this post