NA GOODLUCK HONGO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Tanzania (DCEA) imeendelea na jitihada zake za kulinda afya na usalama wa watanzania kwa kuhakikisha kuwa tatizo la dawa za kulevya nchini linakomeshwa baada ya kumkamata kinara wa biashara hiyo jijini Dodoma.
Hata hivyo sio kazi rahisi kuwakamata ‘mapapa’ wa biashara hizo kutokana na kuwa na mtandao mkubwa wa ndani na nje ya nchi huku wakitumia teknolojia ya hali ya juu katika kufanikisha biashara zao ikiwemo fedha.
Taarifa za kukamatwa kwa anayetuhumiwa kuwa kinara wa biashara ya dawa za kulevya Mkoa wa Dodoma Suleiman Mbarouk Suleiman maarufu kama ‘Nyanda’ ambaye alikuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu bila kukamatwa zimetolewa jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari Novemba 12,2024.
Kukamatwa kwa Nyanda kumekuja miezi miwili baada ya DCEA kumkamata Richard Mwanri anayetuhumiwa kuwa wakala wa dawa za kulevya nchini ambaye amekuwa akipokea dawa hizo kutoka nchi mbalimbali duniani na kuziingiza nchini kwa usafiri wa magari zikiwa zimefichwa kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kisha kuzisambaza .
Akizungumzia kukamatwa kwa Nyanda,Kamishna Jenerali Lyimo amesema DCEA iliwakamata watuhumiwa wawili akiwemo Nyanda na Kimwaga Msobi Lazaro ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Kinyali Kata ya Viwandani wakiwa na gramu 393 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Amesema Nyanda anafahamika kama kinara wa biashara ya dawa za kulevya mkoani humo na amekuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu kabla ya kukamatwa kwake akiwa na dawa hizo za kulevya.
Kamishna Jenerali Lyimo amebainisha kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya nia dhabiti ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kuwa tatizo la dawa za kulevya linakomeshwa ili kulinda afya na usalama wa watanzania.
Amesema mbali na Nyanda lakini pia wamewakamata watuhumiwa wengine 58 katika operesheni iliyofanyika maeneo mbalimbali nchini kuanzia Oktoba na Novemba 2024.
‘’Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini kati ya Oktoba na Novemba 2024 na kufanikiwa kukamata kilogram 1,066.105 za dawa za kulevya ,mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya,na kuteketeza jumla ya ekari 157.4 za mashamba ya bangi na lita 19,804 za kemikali bashirifu.
‘’Uchunguzi umebaini kuwa wateja wengi wa skanka ni wanawake ,ambao hudai kutumia dawa hizo kupunguza msongo wa mawazo na kujistarehesha”amesema Kamishna Jenerali Lyimo
Skanka ni aina ya bangi ya kusindika yenye kiwango kikubwa cha kemikali yenye sumu aina ya Tetrahydrocannabinol (THC) ambayo inaweza kuharibu mfumo wa fahamu, akili na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza kama vile moyo, figo, na ini.
Mbali na skanka lakini pia kuna hashish ambayo hutengenezwa kwa mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi na inapovutwa huzalisha kemikali hatari zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa haraka na mara nyingi jamii huamini kuwa watu wanaopatwa na magonjwa haya wamerogwa.
‘’DCEA inaowamba wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada hizi kwa kufichua wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kuhamasishana kutoshiriki katika biashara na matumizi ya dawa za kulevya.’’amesema Kamshna Jenerali Lyimo
Awali Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Septemba 10,2024 Kamishna Jenerali Lyimo alieleza kuwa wataendela kufanya operesheni mashambani,barabarani na sehemu nyingine na kuwakamata wahusika ili kulinda afya za watanzania.



Discussion about this post