NA GOODLUCK HONGO,LINDI
WAKATI wakazi wa jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania wakiendelea kufuatilia sababu za kutohamishwa kwa kaburi lililopo katikati ya majengo marefu katika eneo la Posta,kaburi lingine la ajabu limeendelea kuacha maswali mengi ndani ya Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Rondo uliopo mkoani Lindi.
Msitu huo ambao unalindwa na kuhifadhiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kuwa eneo maarufu kutokana na kuwa na miti ya asili ambayo haijapandwa na mtu yeyote wala mazingira yake kuhusishwa na binadamu kuyatengeneza.
Mbali na hilo lakini pia watafiti mbalimbali hufika katika msitu huo kufanya tafiti mbalimbali kutoka katika mimea,wanyama na ndege inayopatikana katika eneo hilo pekee duniani.
Mbali na kupatikana kwa miti adimu duniani lakini pia kuna wanyama wasiopatikana sehemu nyingine yoyote isipokuwa katika eneo hilo.
Hata hivyo mbali na kuwa na aina adimu za miti na wanyama,lakini pia kuna kaburi ambalo lipo kati kati ya msitu huo wa mazingira asilia huku likiwa na mlima mdogo ambapo ikitokea umekalia basi sehemu zako zitavimba.
Mbali na hilo lakini pia katikati ya kaburi hilo kuna mti wenye kitambaa ambapo inaelezwa kuwa Chifu huyo alizikwa akiwa amesimama hivyo kuwepo kwa mti huo ni ishara ya eneo kilichopo kichwa chake.
Wenyeji wanaozunguka msitu huo hufika katika kaburi hilo kwa ajili ya kuomba na kufanya matambiko mbalimbali kama ya kuomba mvua.
Bajeti Communication ilifika katika eneo hilo na kujionea jinsi kaburi hilo lilivyo ndani ya msitu mnene uliosheheni miti mikubwa ikiwa na mizizi yenye urefu zaidi ya futi tatu kwenda juu.
Akizungumzia kuhusu kaburi hilo mmoja wa wanakijiji kilichopo karibu na msitu huo John Membe ambesema kaburi ni la miaka mingi zaidi ya 70 iliyopita.
‘’Mimi leo nina miaka 65 na nilizaliwa hapa na kaburi hili lilikuwepo lakini katika kaburi hili kuna kimlima kidogo kama kichuguu sasa kama utakalia pale basi sehemu zako za siri zitavimba.
‘’Kila mwaka huwa tunafanya sherehe kuzunguka kaburi hilo ikiwemo kuomba mambo mbalimbali lakini hakuna anayeweza kukalia pale na kama unavyojua kaburi lilipo ni eneo lenye msitu mkubwa sana’’amesema Membe

Akizungumzia Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia-Rondo,Afisa Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Hifadhi ya Msitu wa Hifadhi ya Mazingira-Rondo John Olomi,amesema hifadhi hiyo ni mojawapo ya hifadhi 23 zilizopandishwa hadhi na kuwa Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia nchini Tanzania.
Amesema ndani ya msitu huo wa hifadhi ya mazingira asilia kuna mimea na wanyama muhimu sana ambayo inapatikana katika eneo hilo pekee na ipo hatarini kutoweka wakiwemo wanyama anayejulikana kwa jina la wenyeji Chinengu(Rondo Galgo dwarf) ambao hawapatikanani duniani zaidi ndani ya msitu huo.
Amesema hifadhi hiyo imepewa nafasi hiyo kwa sababu za huduma nyingi za kiikolojia ikiwemo hali ya hewa na ni hifadhi ya lindimaji ambapo muonekano wake ni eneo lililoinuka kwa maana ya plateau ambapo licha ya kuwepo kwa msitu huo mkubwa lakini hakuna maji yanayopatikana katika eneo hilo.

Akizungumzia kuhusu Kaburi hilo Mhifadhi Olomi amebainisha kuwa
‘’Ndani ya hifadhi yetu tuna kaburi la Chifu Manjonda ambaye alikuwa Chifu wa Kabila la Wamwela na alizikwa katika maeneo hayo ya ndani ya msitu na hilo limekuwa likitoa fursa ya historia nzuri ya kabila hilo linalozunguka hifadhi hiyo,mbali na hilo lakini imebainika katika hifadhi hii kuna mimea na wanyama wanaopatikana katika hifadhi hii ni wale ambao wanawezesha tafiti mbalimbali kufanyika.
‘’Tunawaalika watafiti mbalimbali wanaopenda kufanya tafiti kuja ndani ya hifadhi yetu kwani bado tuna utajiri mkubwa wa mimea pamoja na wanyama ambao hawapatikani sehemu nyingine zaidi ya maeneo haya.
‘’Tunawaalika wananchi na wageni wetu kutoka maeneo mbalimbali kuja kwenye hifadhi yetu ya Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia-Rondo kwa ajili ya kufanya shughuli nyingi za kiutalii kwani bado msitu wetu una hifadhi kubwa ya mazingira asilia ya kufanya shughuli za kitalii”ameongeza Olomi
Naye Afisa Uhifadhi wa Msitu huo Ahazi Shayo ameongeza kuwa hifadhi inazungukwa na vijiji sita ambavyo kabila kuu katika eneo hilo ni Wamwela.

Amesema Chifu Manjonda alihamia katika eneo la Rondo kutoka nchini Msumbiji na baada ya kukaa miaka mingi na wenyeji ndipo walipompa uchifu.
‘’Baada ya kufariki ndio alizikwa hapa katika msitu na hapa huwa wanakuja kusafisha ili liendelee kuonekana kwa kuwa lipo ndani ya msitu mkubwa na huja kwa ajili ya kuomba mambo mbalimbali.
‘’Sisi tunashirikiana nao kuhakikisha kuwa Msitu wetu unaendelea kubakia wa asili na kimlima hiki kinachoonekana katika kaburi ni kwamba hutakiwi kukikalia na ikitokea umekikalia basi utavimba na hilo ni kwa mujibu wa kabila la Wamwela,hivyo kila wanapokuja kuomba hapa hakuna mtu anayekalia eneo hili’’amebainisha Shayo




Discussion about this post