NA MWANDISHI WETU,SONGWE
JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe limethibitisha kutokea kwa ajali ya barabarani iliyohusisha gari T. 958 BCS aina ya Scania na Bajaji yenye namba MC. 783 DUF aina ya TVS na kusababisha vifo vya watu watano.
Ajali hiyo imetokea Novemba 22, 2024 majira ya saa 3:15 usiku ambapo bajaji hiyo ilikuwa ikitokea barabara ya Mji mdogo wa Mpemba na kuelekea Mji wa Tunduma na kujaribu kuyapita magari mengine yaliyokuwa mbele yake kisha kugongana na gari hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 23,2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe SACP- Augustino Senga amesema Bajaji hiyo ilikuwa ikiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Hakimu Kalinga Mkazi wa Muungano Mjini Tunduma na kusababisha vifo vya watu watano akiwemo dereva wa Bajaji hiyo.
Kamanda Senga amewataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni, Emmanuel Hakim Kalinga ambaye alikuwa Dereva wa Bajaji, Rehema Christopher Sikamnga, (25) na mkazi wa Msongwa, Festo Aron Mambwe (57) Mkristo Msafwa mkazi wa Mbeya, Rosemary Njema (44) mkazi wa Ipito Tunduma na Milembe Siyantemi (36) mkazi wa Kapele.
Marehemu hao wamehifadhiwa katika Kituo cha Afya Tunduma kilichopo Wilaya ya Momba na chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa ambapo Dereva wa Scania anatafutwa.
”Jeshi la Polisi Mkoa Songwe linatoa wito kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kukagua vyombo vyao kabla ya kuanza safari na kuzingatia sheria za usalama barabarani wakati wote”amesema Kamanda Senga



Discussion about this post