NA MWANDISHI WETU,MTWARA
CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika miezi michache ijayo unakuwa huru,haki na amani.
CUF imetoa wito huo wakati kukiwa na vuguvugu la kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika miezi michache ijayo wakati vyama vingine kikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiendelea na zoezi la kutoa fomu kwa wanachama wake kwa ajili ya nafasi za ubunge na udiwani kabla ya kupata mgombea mmoja wa nafasi hizo.
Akizungumza na Bajeti Communication mkoani Mtwara Julai 2,2025,Mkurugenzi wa Habari,Uenezi na Mahusiano kwa Umma wa CUF Mhandisi Mohamed Ngulangwa amesema kwa sasa CUF inaendelea na mchakato wa ndani kwa ndani wa kutoa na kurudisha fomu kwa wanachama wake.
Amesema ifikapo Julai 15,2025 itakuwa ndio mwisho wa wanachama wao kuchukua na kurudisha fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi za ubunge na udiwani katika maeneo yote nchini.
“Sisi tutashiriki uchaguzi wala hatutasusia,kwani mwaka 2015 tulisusia uchaguzi wa marudio kule Zanzibar baada ya kufutwa uchaguzi wa kwanza na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) Jecha Salim Jecha.
“Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan na vyombo vingine vinavyohusika na uchaguzi kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa huru,haki na wa amani”amesema Mhandisi Ngulangwa
Mhandisi Ngulangwa amebainisha kuwa wao hawafanyi siasa za ‘lipstick’ kwamba kila kinachofanyika lazima kiwe wazi kwa vyombo vya habari lakini baada ya kumaliza zoezi lao la mchakato wa wa ndani wa kuwapata wagombea wao ndipo wataanza kuwatangaza rasmi.




Discussion about this post