NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA),ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Kilimo; ilianzishwa kwa Sheria ya Mbolea Namba. 09 ya Mwaka 2009 (Fertilizer Act, No.9 of 2009) na kanuni zake za Mwaka 2011.
Majukumu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania yameainishwa chini ya kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mbolea.
Aidha, Mamlaka ilianza utekelezaji wa majukumu yake mnamo Agosti 2012. Katika kutekeleza majukumu yake,kwa mujibu wa Kifungu cha 4(1)(0) cha Sheria ya Mbolea Na. 9 ya mwaka, 2009,
Mamlaka ilikasimiwa jukumu la kusimamia Mpango wa Ruzuku ya Mbolea kwa lengo la kuwapunguzia wakulima gharama ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwanda.
Utoaji wa ruzuku unazingatia mahitaji halisi ya mkulima kulingana na taarifa za usajili na bajeti ya Serikali iliyotengwa ambapo mpango huo unahusisha mbolea za kupandia na kukuzia.
Katika miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Kilimo nchini,hususani kwenye tasnia ya mbolea kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
Kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea ulioidhinishwa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mbolea inapatikana kwa bei nafuu kwa kutumia mfumo wa kidijiti wa mbolea, wakulima sasa wanapata mbolea kwa bei iliyopunguzwa, jambo ambalo limeongeza matumizi ya mbolea nchini.
Aidha, Serikali imewekeza katika kuimarisha usambazaji wa mbolea kwa wakulima hasa katika maeneo ya vijijini, ambako wakulima wengi wanategemea kilimo kwa ajiliya maisha yao.
Serikali kupitia TFRA inaendelea kuratibu upatikanaji wa mbolea nchini kwa kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima hadi mwaka 2025/2026 ili kuongeza matumiziya mbolea (per capital consumption) kutoka kilo 19 kwa hekta hadi angalau kilo 50 kwa hekta na kuwapunguzia gharama za uzalishaji wakulima.
Hata hivyo TFRA inaendelea kuratibu uingizaji wa mbolea nchini ambapo mpaka mwezi Disemba 2024, kiasi cha tani 494,075 kilikuwa kimeingizwa nchini ikiwa ni asilimia 60.2 ya lego la kuingiza tani 750,000 ifikapo Juni, 2025.

Kwa upande wa hali ya upatikanaji wa Mbolea na Visaidizi vya mbolea ulikuwa hadi kufikia Disemba, 2024 ulikuwa ni tani 803,087 sawa na 80 ya makisio ya mahitaji ya mwaka ambayo ni tani milioni moja.
Ruzuku ya Mbolea kwa Wakulima Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent anaeleza kuwa, tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, ameonesha dhamira ya dhati ya kuinua Sekta ya Kilimo na hivyo kuamua kutoa ruzuku ya mbolea baada ya kubaini changamoto za bei ya mbolea kwamwaka 2021/2022 zilizotokana na mlipuko wa Uviko- 19 na Vita kati ya Urusi na Ukraine hali iliyopelekea wakulima kushindwa kumudu bei ya mbolea.
Anasema Serikali ilianza kutoa ruzuku hiyo msimu wa kilimo wa 2022/2023 na imedhamiria kutoa mpaka ifikapo Mwaka 2025/2026 baada ya bei ya mbolea kuimarika kwenye soko la dunia pamoja na kuongeza matumizi ya mbolea zinazozalishwa na viwanda vya ndani.
Laurent anasema, kupitia utekelezaji wa mpango wa utoaji wa ruzuku ya mbolea, Wizara kupitia Mamlaka imepanga kuongeza matumizi ya mbolea kutoka kilo 19 hadi kufikia kilo 50 kwa hekta ifikapo mwaka 2030.
Anaongeza kuwa, hali ya upatikanaji wa mbolea kwa Mwaka 2021/2022 ilikuwa tani 560,551 huku matumizi yakiwa tani 462,496.
“Hadi kufikia mwezi Desemba 2024, hali ya upatikanaji wa mbolea na visaidizi vyake ilikuwa tani 803,087 sawa na asilimia 80 ya mahitaji ya wakulima ya tani 1,000,000.
“Utekelezaji wa ruzuku ya mbolea kumepunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija kwa wakulima ambapo uzalishaji wa mazao umeongezeka kutoka tani milioni 30.4 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 36 mwaka 2023/24”anasema Laurent.
Aidha anaongeza kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani milioni 17 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 20 mwaka 2022/23 ambapo pamoja na manufaa yatokanayo na
utekelezaji wa mpango wa ruzuku ya mbolea, imepelekea kuongezeka kwa mtandao wa usambazaji wa pembejeo za kilimo hadi kufikia ngazi ya kata kufuatia uwepo wa fursa ya biashara ya mbolea kupitia mawakala wa usambazaji wa mbolea za ruzuku nchini.
“Hali hiyo imepelekea vituo vya usambazaji nchini kuongezeka kwa vituo vya mawakala wa usambazaji wa mbolea kutoka 1,772 mwaka 2022/23 hadi kufikia vituo 6,847 vya usambazaji”anabainisha Laurent

Akizungumzia mfumo unaotumika katika kusambaza mbolea za ruzuku nchini ambao kwa sasa unatumika pia kusambaza ruzuku ya mbegu za mahindi,
Meneja wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Robert Mtendamema anasema, Serikali imefanikiwa kuja na mfumo wa kidijitali unaotumika katika kutekeleza mpango wa mbolea za ruzuku toka kuanza kwa utekelezaji wake mwaka 2022/2023.
Anasema kuwa, mfumo unaotumika ni rafiki na umeiwezesha serikali kuwatambua wazalishaji, waingizaji na wafanyabiashara wakubwa wa mbolea, wakala wa mbolea na mkulima mmoja mmoja na ukubwa wa shamba analolima, na hivyo kuwezesha kuweka mipango ya kusimamia mwenendo wa Sekta ya Kilimo kwa uhakika zaidi.
Anaeleza kuwa, hadi kufikia mwezi Desemba 2024 waingizaji wa mbolea 28 wamesajiliwa, wazalishaji watatu, mawakala na wasambazaji wa mbolea 6,847 wamesajiliwa watakaotumika kusambaza mbolea katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
“Kufuatia uwepo wa mazingira rafiki ya biashara ya mbolea ndani ya nchi, idadi ya wafanyabiashara wa Mbolea imeongezeka kutoka wafanyabiashara 1,691 mwaka 2020/2021 hadi kufikia wafanyabiashara 4,776 Desemba 2024.
“Kufikia Desemba 30, 2024 jumla ya wakulima 4,213,951 walikuwa wamesajiliwa kwenye mfumo wa kidijiti wa Ruzuku ya Mbolea, ambao ni sawa na asilimia 60.2 ya lengo la Serikali la kusajili wakulima milioni saba ifikapo mwaka 2026”anabainisha Mtendamema
Aidha,anafafanuwa kuwa vituo 4,801 vya usambazaji wa mbolea vimesajiliwa kote nchini, huku mawakala wakisajiliwa na kuwezeshwa kufanikisha usambazaji wa mbolea kwa ufanisi.
Katika msimu wa kilimo 2022/2023, jumla ya tani laki 386.3 zenye thamani ya ruzuku ya Sh.Bilioni 370.9 zilinunuliwa na wakulima kupitia mpango wa ruzuku.
Mtendamwema anaongeza kuwa jumla ya tani laki 515.8 zenye thamani ya ruzuku ya Shilingi Bilioni 151 zilinunuliwa na wakulima katika mpango wa ruzuku kwa msimu wa kilimo wa 2023/2024, na kufanya jumla ya thamani ya ruzuku kwa misimu ya 2022/2023 na 2023/2024 kufikia kiasi cha Shilingi Bilioni 521.5.
“Uwepo wa mfumo huu wa Kidijitali wa pembejeo ya ruzuku umewezesha Serikali kuwa na kanzidata au takwimu za wakulima zinazoaminika.
“Kupitia kanzidata hiyo, Serikali inaweza kupanga mikakati sahihi ya kuinua sekta ya kilimo.
“Kufuatia mafanikio yaliyopatikana kupitia matumizi ya mfumo wa kidijiti wa mbolea katika kutoa ruzuku za mbolea, serikali imeridhia mfumo huo utumike pia katika kutoa ruzuku ya mbegu za mahindi zinazotolewa kuanzia msimu wa kilimo wa 2024/2025 ili kumrahisishia mkulima namna ya kupata mbembejeo hizo za kilimo”anabainisha Mtendamwema.
Kuimarika kwa Udhibiti wa Mbolea Nchini
Akizungumzia kuhusu udhibiti wa pembejeo ya mbolea, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Elizabeth Bolle anasema, mifumo ya udhibiti wa mbolea nchinimimeendelea kuimarishwa ili kuhakikisha wakulima wanapata mbolea bora kwa bei nafuu na kwa wakati.
Anasema shughuli za udhibiti zimewezekana kwakuongeza idadi ya wakaguzi wa mbolea, kuwasajili wafanyabiashara wa mbolea, na kutoa mafunzo juu ya uendeshaji wa biashara ya mbolea kwa wafanyabiashara wa mbolea nchini.
Anaeleza kufuatia uwezeshwaji unaofanywa na Rais Dkt. Samia kumekuwa na ongezeko la wakaguzi wa mbolea 140 kutoka katika Ofisi za Mamlaka na Halmashauri za Wilaya.
Aidha ameongeza kuwa, Maafisa Kilimo 100 kati ya 140 walipata mafunzo ya ukaguzi na tayari wametangazwa kwenye gazeti la serikali tayari kwa kuendelea na jukumu la kudhibiti ubora wa mbolea katika maeneo yao.
Uchunguzi wa Maabara na Usajili wa Mbolea
Ndani ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, TFRA imepewa bajeti ya kutekeleza ujenzi wa Maabara ya Mbolea kwa njia ya Force Account ambapo ujenzi wake umekamilika na shughuli za upimaji wa sampuli za mbolea unaendelea.
Uwepo wa Maabara ya Mbolea umeongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka na inatarajiwa kutumiwa na nchi jirani za Malawi, Zambia, DRC, Burundi na Rwanda, na hivyo kuongeza mapato ya nchi.
Mbolea mpya 95 (11 granule na 84 mboleo za mji folier) zimesajiliwa na kuwekwa kwenye tovuti ya Mamlaka kwa uwazi na urahisi wa upatikanaji wa taarifa.
Utoaji wa Leseni
Kwa upande wa utoaji wa leseni,zaidi ya wafanyabiashara 977 wamesajiliwa kufikia Machi 2024, wakijumuisha Kanda ya Mashariki wakifikia 174,Kanda ya Ziwa 107,Kanda ya Kaskazini 96,Kanda ya Kati 144, na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini 456.
Maendeleo ya Viwanda vya Mbolea
Akizungumzia maendeleo ya Viwanda vya Mbolea nchini,Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji wa Ndani na Uingizaji wa Mbolea kwa Pamoja wa TFRA, Louis Kasera, anaeleza kuwa kufuatia utashi wa kisiasa na uhamasishaji uliofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na ongezeko la viwanda vinavyozalisha aina mbalimbali za mbolea na visaidizi vyake nchini, kufikisha idadi ya viwanda 23.
Anasema kati ya viwanda hivyo, vitatu huzalisha visaidizi vya mbolea (chokaa mazao na gypsum) vilivyoko mikoa ya Dodoma na Tanga, na viwanda 20vinatengeneza mbolea za punje na maji, ambapo kati ya hivyo 11 hutengeneza mbolea za maji na sita hutengeneza mbolea za punje.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali ya Rais Dkt Samia imeendelea kuhamasisha Sekta Binafsi katika kuwekeza, ambapo mwekezaji kutoka nchini Burundi yupo katika hatua za mwisho za ujenzi wa kiwanda cha Itracom Fertilizer LTD kilichojengwa Nala Jijini Dodoma, ambacho tayari kimeanza uzalishaji wa tani 200,000 kwa mwaka.
“Baada ya mitambo yote kukamilika, kiwanda kitazalisha tani milioni moja za mbolea na tani 300,000 za chokaa, na hivyo kusaidia kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi”anasema Kasera
Mazingira Mazuri ya Sera na Uongozi
Sera bora za kilimo ni nguzo muhimu ya Maendeleo ya Tasnia ya Mbolea ambapo Rais Dkt.Samia ameonesha dhamira ya dhati ya kuondoa vikwazo vya kikodi vinavyoathiri bei ya mbolea.
Aidha, uboreshaji wa miundombinu ya barabara, reli, na bandari ni hatua muhimu inayowezesha usambazaji wa mbolea kufanyika kwa haraka na kwa gharama nafuu.
Hitimisho
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonesha dhamira ya dhati ya kuboresha Sekta ya Kilimo, hususani kupitia usimamizi wa tasnia ndogo ya mbolea.
TFRA itaendelea kuhamasisha uwekezaji, kuhakikisha upatikanaji wa mbolea zenye viwango vilivyothibitishwa na Mamlaka, na kufanikisha mageuzi ya kiuchumi kupitia kilimo.
Hatua hizi zinathibitisha kuwa Uongozi wa Rais Dkt. Samia umejikita katika kuboresha maisha ya wakulima na kuinua ustawi wa Taifa kwa ujumla.




Discussion about this post